Featured Michezo

GEKUL AZITAKA HALMASHAURI NCHINI KUHAMASISHA PROGRAMU YA JOGGING MTAA KWA MTAA

Written by mzalendoeditor

Na. John Mapepele

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Pauline Gekul amezitaka Halmashauri zote nchini kuhamasisha programu ya kufanya mazoezi kuanzia ngazi ya mtaa ili kuimarisha afya kwa jamii na kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan za kuibua vipaji vya michezo kuanzia ngazi ya chini.

Mhe. Gekul amesema hayo leo Februari 20, 2022, alipokua Mgeni Rasmi kwenye kilele cha Bonanza kubwa lililoandaliwa na Umoja wa Vilabu vya jogging klabu Mbagala, Mtoni Kijichi jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza mbio za takribani kilomita 7.5 kuanzia Mbagala hadi Mtoni Kijichi.

Amezitaka Klabu za Mazoezi kote nchini kuhakikisha zinashirikisha kikamilifu makundi maalum ya jamii kwenye siku za mazoezi, huku akitoa pongeza kwa umoja wa Mbagala Jogging Klabu kwa kuandaa tamasha hilo ambalo amelielezea kuwa limekuwa la mafanikio makubwa.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote kutenga muda kila siku kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.

“Akina mama wenzangu ujanja ni kufanya mazoezi ili kuboresha afya na mazoezi.” Ameongeza Mhe. Gekul

Aidha, amezitaka Halmashauri zote nchini zikumbuke kutenga fedha kwa ajili ya michezo kwenye bajeti ya mwaka 2022/23 ili zisaidie shughuli za Michezo.

Katika hatua nyingine Mhe. Gekul ametoa rai kwa wanamuziki kuacha mara moja tabia ya kuingiza vionjo kwenye Wmbo wa Taifa kwani kwa kufanya hivyo wanaondoa uhalisia wa wimbo huo.

Tamasha hilo limebebwa na ujumbe “Michezo, Afya Uchumi na ndoa.

About the author

mzalendoeditor