Featured Kitaifa

MWANAMKE ALIYETOLEWA FIGO NA MWAJIRI WAKE KULIPWA MAMILIONI

Written by mzalendoeditor

Mfanyakazi wa ndani kutoka nchini Uganda, Judith Nakintu ambaye siku chache zilizopita aligundulika kutolewa figo bila ridhaa yake na mwajiri wake nchini Saudi Arabia, atalipwa fidia ya Riyal 271,450 ambazo ni takribani shilingi milioni 167.4 za Kitanzania.

Mahakama nchini Saudi Arabia, imemuamuru mwajiri wake, Saad Dhafer Mohamed Al- Asmari kulipa fidia hiyo, baada ya kubainika kwamba hausigeli huyo alitolewa figo katika mazingira yenye utata katika Hospitali ya King Fahad, Jeddah nchini Saudi Arabia akiwa chini ya mwajiri huyo.

Siku chache zilizopita, madaktari katika Hospitali ya Mulago nchini Uganda, walithibitisha kwamba mwanamke huyo alitolewa figo yake ya kulia, ambapo muda mfupi baadaye, polisi nchini humo walianza kulishughulikia suala hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kimataifa ili kuwatia hatiani wote waliohusika na tukio hilo.

Wamiliki na mameneja wanne wa kampuni ya Nile Treasure Gate yenye makao makuu yake Kampala nchini Uganda ambao ndiyo waliohusika kumsafirisha mwanamke huyo kwenda Uarabuni, tayari wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

About the author

mzalendoeditor