Featured Kitaifa

NI MUHIMU KULINDA MAENEO OEVU KWA KUEPUKA KUANZISHA UJENZI – NEMC

Written by mzalendoeditor


BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC) limeiagiza Halmashauri ya Mji wa Kibaha kufanya tathimini ya kimazingira ya Kimkakati katika bonde la Mto Ruvu ambapo kumependekezwa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule.

Kufanya hivyo ni kuepusha athari zinazoweza kusababishwa na shughuli za kibinadamu katika eneo hilo zikiwemo za ujenzi ambazo husababisha kukauka kwa vyanzo vya maji.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza hilo Dk Samuel Gwamaka mara baada ya kutembelea baadhi ya maeneo ya bonde la Mto Ruvu kwa lengo la kujionea hali halisi ya uhifadhi sambamba na kufanya tathimini ya baadhi ya maeneo ambayo halmashauri ya Mji wa Kibaha ilikusudia kufanya ujenzi wa shule.

” Nimekagua maeneo mbalimbali yaliyopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa shule katika Halmashauri hii na kubaini kuwa maeneo hayo yapo katika maeneo oevu katika chanzo cha chamaji cha Mto Ruvu.S ote tunatambua kuwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani mategemeo yao wote ya maji ni kutoka katika bonde hili la Mto Ruvu hivyo tunapaswa kulitunza kwa nguvu zote” alisema Dk Gwamaka.

Alisema hata jengo la Halmashauri ya Mji huo limejengwa katika eneo Oevu hali iliyolifanya likabiliwe na changamoto katika mifumo yake ya maji taka huku akisisitiza kwa wadau wote wakiwemo wawekezaji kusubiri ripoti ya athari za kimazingira katika eneo hilo kabla ya kufanya ujenzi wowote.
“Wote tunajua kuwa maji yanatoka katika milima hasa kipindi cha mvua, sehemu ambayo ni hifadhi yake hata kama kuna mafuriko ni maeneo kama haya ambayo kama yasipotunzwa athari zake ni kubwa, changamoto inayojitokeza ni msukumo wa maendeleo kama ilivyo kwa Kibaha ambayo inataka kujenga shule ndani ya maeneo hayo jambo ambalo ni hatari kwa mazingira haya” alisisitiza Dk Gwamaka

Aliwataka wadau wote wa kimaendeleo kusubiri ripoti ya tathimini ya kimkakati inayofanyiwa kazi na Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo itatoa majibu kuwa kama eneo hilo linafaa kwa ujenzi wa makazi au viwanda.
Awali Afisa Mazingira wa Halmashauri wa Mji wa Kibaha Maximilian Mtobu alisema wao kama taasisi ya Serikali wamepokea maagizo ya NEMC kwa umakini mkubwa kwa kuwa ndiyo taasisi inayotambua athari za kimazingira nchini yakiwemo maeneo ambayo walikusudia kufanya ujenzi huo
Alisema baada ya tathimini iliyofanywa na Baraza hilo ambayo imepinga ujenzi wa shule katika maeneo waliyokuwa wamekusudia, watakaa na kujadili ili kuangalia ni wapi watafanya ujenzi huo ili pamoja na mambo mengine kuufanya ujenzi huo kuwa wa kudumu na wenye manufaa kwa Taifa.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utekelezaji na Uzingatiaji wa sheria Mhandisi Redempta Samuel, amesema kuwa zipo changamoto ambazo wameziona katika maeneo pendekezwa ya kujenga shule ambazo zina atahri kimazingira .

Moja ya changamoto hizo ni kuwa maeneo yotehayo yako katika maeneo oeve, (maeneo lindwa), changamoto ingine ni mojawapo ya eneo kupakana na bonde amabalo ni chanzo cha maji.

About the author

mzalendoeditor