Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amewapongeza wawakilishi wa Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) kwa mkakati wao wa kutoa elimu kwa viongozi na wananchi wa Mkoa huo hasa katika maeneo ambayo utafiti wa mafuta unafanyika.
Akitoa pongezi hizo leo 16 Februari 2022 ofisini kwake Dkt. Mahenge amesema endapo tafiti ambazo wanaendelea nazo zitakuwa na matokeo chanya zitasaidia kuongeza pato la taifa kupitia uuzaji wa mafuta na gesi ambayo yameonekana katika baadhi ya maeneo ya Singida na baadhi ya mikoa ya jirani.
Aidha amewahakikishia wataalamu hao kwamba Serikali ya mkoa itatoa ushirikiano wote utakaohitajika katika kufanikisha utafiti huo kwa kuwa miradi hiyo ikikamilika itakuwa na manufaa makubwa kwa wanachi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Awali akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa Mtaalamu wa utafiti wa mafuta na gesi Habibu Mohamedi kutoka Shirika hilo amesema Shirika linafanya utafiti katika kitalu cha Eyasi Wembere kilichopo Kaskazini – Mashariki mwa Tanzania ndani ya bonde la ufa la Afrika Mashariki.
Habibu amesema bonde la Eyasi – Wembere ni moja ya maeneo muhimu yenye miamba tabaka yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta na gesi asilia ambalo linapita katika mikoa mitano ya Tabora Singida Arusha Simiyu na Shinyanga.
Aidha Habibu amebainisha kwamba shughuli za utafutaji wa mafuta /gesi asilia katika kitalu hicho zilianza mwaka 2015 ambapo kampuni ya taifa ya mafuta (TPDC) ilikusanya taarifa za awali za kijiofizikia zenye urefu wa Km.11,323 za mstari.
Kutokana na tafiti hizo Bw. Habibu alieleza kwamba kati ya mwaka 2019/2020 visima vifupi vya utafutaji wa mafuta/gesi asili vilichimbwa ili kubaini aina ya matabaka ya miamba hiyo.
Hata hivyo ameendelea kubainisha kwamba katika mwaka wa fedha wa 2021/22 shirika limepanga kufanya utafiti wa kijiokemia kwa lengo la kuangalia uwezekano kupata mafuta/gesi ambapo mikoa ya Singida Tabora Shinyanga Arusha na Simiyu itafanyiwa utafiti huo.
Kwa upande wake afisa mahusiano wa shirika hilo Deliani Kabwogi akafafanua kwamba mradi huo ni muhimu kwa taifa na mkoa kwa ujumla kwa kuwa kuongeza kipato na utasaidia upatikanaji wa ajira za muda mfupi wakati wa kusafisha mikuza, kulinda mashine na vifaa vitakavyotumika kwenye utafiti, huduma za malazi na chakula.
Deliana akafafanua kwamba upatikanaji wa mafuta /gesi katika eneo hilo utawezesha nchi kuwa na uhakika wa nishati ya mafuta au gesi na kuongeza mapato kupitia mauzo ya nishati ambayo yatasidia kuchangia uboreshaji huduma za kijamii.