Featured Kitaifa

RAIS SAMIA:’TANZANIA KUTENGENEZA CHANJO ZAKE ZENYEWE’

Written by mzalendoeditor

  

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel mara baada ya kuwasili katika Makao Makuu ya Baraza hilo Brussels nchini Ubelgiji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel mara baada ya kuwasili katika Makao Makuu ya Baraza hilo Brussels nchini Ubelgiji

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa amewasili katika chumba cha Mkutano kwa ajili ya mazungumzo na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel leo tarehe 15 Februari, 2022 katika Makao Makuu ya Baraza hilo Brussels nchini Ubelgiji.

PICHA NA IKULU

……………………………………………………..

Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake ina mipango ya kuanzisha kiwanda cha kuzalisha chanjo za COVID-19 na maradhi mengine ndani ya nchi.

Katika mazungumzo yake  na Mhe. Charles Michel, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (European Council) wakati wa ziara yake rasmi nchini Ubelgiji, Rais Samia amesema kuwa bajeti ya serikali ya Tanzania kununua chanjo inakadiriwa itaongezeka kutoka shilingi bilioni 26.1 mwaka 2020 hadi bilioni 216 ifikapo mwaka 2030, ambayo ni sababu muhimu ya kujenga kiwanda hicho.

‘Tanzania inaomba kuwasilisha mapendekezo, natarajia mtawezesha wazo hili kuwa mradi wenye manufaa. Naamini mpango huu utakapotekelezwa utafungua fursa mpya za kuimarisha mahusiano yetu.’

Tangu kuanzishwa rasmi kwa ushirikiano mwaka 1975, Tanzania imepokea zaidi ya Euro bilioni 2.3 ambayo ni sawa na shilingi trilioni 5.98. Tangu wakati huo, Umoja wa Ulaya umebaki washirika wa kimkakati na wa kimaendeleo kwa Tanzania.

Wakati huo huo, Rais Samia ameusihi Umoja wa Ulaya kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya nchi jirani ya Burundi kuimarisha mazingira ya ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa Umoja huo una ushawishi mkubwa  hata kwa Jumuiya nyingine za kimataifa kuunga mkono juhudi za kuleta utulivu na maendeleo.

‘Burundi tulivu ina manufaa kwa maeneo ya Maziwa Makuu, nzuri kwa Umoja wa Ulaya na duniani kwa jumla’.

About the author

mzalendoeditor