Featured Michezo

Polisi, Yanga kukipiga Sheikh Amri Abeid Arusha

Written by mzalendo

Mchezo huo ulipangwa kupigwa Jumapili katika uwanja wa Ushirika lakini siku moja kabla ya mchezo yani Jumamosi kutakuwa na tamasha la Utamaduni Mkoa wa Kilimanjaro ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hivyo imeilazimu uongozi wa timu hiyo kuhamishia mechi hiyo Arusha.

Inaweza kuwa ni habari njema kwa Yanga kwani wenyewe wameweka kambi jijini hapa kujiandaa na mchezo huo na tayari juzi wametumia uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwa mechi moja ya kirafiki dhidi ya Mbuni FC inayoshiriki ligi daraja kwanza (First league), ambapo timu hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Makamu mwenyekiti wa Polisi Tanzania FC, Robert Munisi amesema awali walipanga kutumia uwanja wao wa nyumbani wa Ushirika katika mchezo huo lakini baada ya kuona itatumika kwenye matamasha la Utamaduni wameona wahamie Arusha ambapo itatoa urahisi kwa wapenzi wao kujitokeza kwa wingi na kuisapoti timu.

Alisema athari za kuhamishia mchezo huo jijini Arusha kutoka Moshi ni kubwa sana kwa sababu Ushirika ni uwanja ambao wameizoea pia maandalizi tayari walishafanya ya kucheza hapo ikiwemo kuboresha sehemu ya kuchezea (pitch), na sasa wanaenda katika uwanja mwingine ambao nao watakuwa kama wageni.

“Katika kanuni mnaulizwa kama ikitokea dharura uwanja wenu wa pili ni upi na sisi uwanja wetu wa pili ni Sheikh Amri Abeid tunakwenda kupambana kushinda hili kubakisha alama tatu nyumbani “

“Tumefanya jitihada zote za kuhakikisha mchezo huo unasogezwa mbele lakini mpaka asubuhi ya leo jitihada hizo zimeshindikana sasa tunasubiri taarifa rasmi kutoka bodi ya ligi lakini asilimia za kwenda kucheza Arusha ni kubwa” amesema Munisi.

Ameongeza kuwa wanatambua Yanga tayari jijini Arusha wamekuwa kama wenyeji hasa baada ya kuweka kambi na kupata nafasi ya kutumia uwanja ambao utapigwa mchezo huo lakini na wao wala hawana wasiwasi kwani timu hiyo haina historia ya kushinda dhidi ya kushinda ugenini.

Makamu katibu wa Yanga tawi la Mkoa wa Arusha, Maulid Rashid yeye anasema kuletwa kwa mchezo huo jijini hapa ni fursa kwa mashabiki wao wengi kutoka mikoa jirani ya Kilimanjaro, Manyara na Singida kuweza kujitokeza kwa wingi na kuiunga mkono.

Amesema Polisi Tanzania ni timu nzuri ina wachezaji wengi wazoefu ndio maana inashika nafasi ya nne katika msimamo lakini kutokana na usajili ambao Yanga imefanya dirisha dogo na namna kikosi kilivyo kwa sasa kama shabiki anaamini watazichukua tu hizo alama tatu bila wasiwasi.

Mara ya mwisho Polisi Tanzania kucheza na Yanga katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid ilikuwa ni Machi 7 mwaka 2021 ambapo timu hizo zilitoka sare ya kufungana goli 1-1. Bao la Yanga likifungwa na Fiston Abdul Razak dakika 42 huku la Polisi likifungwa na Pius Buswita dakika ya 89.

Katika msimamo wa Ligi Kuu NBC Yanga ndio vinara kwa alama 32 baada ya michezo 12, imeshinda 10, sare mbili, ikiwa imefunga mabao 22 na kufungwa goli nne pekee, utofauti ya alama 14 na Polisi Tanzania inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo kwa alama 18.

About the author

mzalendo