Mbeya. Mbeya City imeendelea kutakata katika uwanja wake wa nyumbani baada ya leo tena kuwapapasa Ruvu Shooting bao 1-0 katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu.

Kabla ya mchezo huo, timu hiyo ilikuwa na kumbukumbu ya kuichachafya Simba ushindi kama huo na leo tena ikazidi kujiimarisha nafasi ya tatu kwa pointi 23 kwa kuwachapa Maafande hao.

Katika mchezo huo ambao umepigwa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, ukighubikwa na utelezi kutokana na mvua iliyonyesha na kusababisha kukosekana ladha ya mechi hiyo kwa mashabiki.

Ruvu Shooting walionesha uwezo wao, lakini mbali na uwanja kutokuwa rafiki kwa timu zote walikosa umakini katika kutumia nafasi walizopata ikiwamo penalti waliyokosa dakika ya 55 kupitia kwa Renatus Kisasi baada ya shuti lake kugonga nguzo na kuokolewa na mabeki wa Mbeya City.

Ilikuwa dakika ya 53, Azizi Andabwile alipoiandikia bao la kuongoza Mbeya City akitumia vyema kichwa chake kuingiza mpira wavuni kufuatia mpira wa kona uliochongwa na Richardson Ng’ondya.

Hata hivyo, Ruvu Shooting walijikuta wakicheza pungufu baada ya mchezaji wao, Abdulswamad Kassim kuoneshwa kadi nyekundu kutokana na makosa aliyofanya kwa nyakati tofauti zilizozaa kadi mbili za njano na mwamuzi, Ramadhan Kayoko kumuonesha nyekundu.

Mbeya City walionekana kutakata zaidi kwa kutengeneza mashambulizi mengi lakini hali haikuwa nzuri sana kuweza kuongeza idadi ya mabao hadi dakika 90 kumalizika.

Matokeo hayo yanaifanya Mbeya City kubaki nafasi ya tatu kwa pointi 22 nyuma ya Simba yenye alama 24, huku Wazee wa Mpapaso wakibaki nafasi yao ya 14 kwa alama 11 baada ya timu zote kucheza mechi 13.

Previous articlePolisi, Yanga kukipiga Sheikh Amri Abeid Arusha
Next articleIGP SIRRO AWAVALISHA NISHANI MAOFISA, WAKAGUZI NA ASKARI 123

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here