Featured Kimataifa

RAIS RUTO APONGEZA UBUNIFU WA WAJASIRIAMALI WA TANZANIA KATIKA MAONESHO YA JUA KALI

Written by Alex Sonna

 

Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto akiangalia bidhaa za Wajasiriamali wa Tanzania katika alipotembelea Maonesho ya 25 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali, yanayofanyika Nairobi, Kenya tarehe 11 Novemba, 2025 wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo.

Na. OWM (KVAU) – Nairobi

Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto amepongeza Wajasiriamali wa Tanzania kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora na ubunifu wakati alipotembelea mabanda ya wajasiriamali wa Tanzania katika Maonesho ya 25 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, maarufu kama Nguvu Kazi/Jua Kali, yanayofanyika jijini Nairobi.

Aidha, Rais Ruto ametoa pongezi hizo Novemba 11, 2025 wakati akifungua rasmi maonesho hayo na kuwataka wajasiriamali wa nchini Tanzania kuendelea kushirikiana na wajasiriamali wa Kenya na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu za kutengeneza bidhaa na kutafuta masoko ndani ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki sambamba na mataifa mengine.

Vile vile, amesema dhamira ya Marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kutatua vikwazo visivyo vya kiforodha vinavyoendelea kuzuia biashara katika maeneo ya mipakani.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Alana Nchimbi amesema kuwa maonesho hayo yameendelea kuwawezesha wajasiriamali Wadogo na wa Kati wanaojihusisha na shughuli za kiuchumi katika sekta isiyo rasmi kurasimisha shughuli zao na kuwapatia fursa ya kutangaza bidhaa zao, kubadilishana taarifa, kukuza ujuzi pamoja na kukuza masoko ya bidhaa na huduma.

Kwa upande mwengine, Wajasiriamali hao wameonyesha furaha baada ya pongezi hizo na kueleza kuwa wataendelea kutumia fursa hiyo kujitangaza, kupata masoko mapya na kujifunza mbinu bora za biashara kutoka kwa wenzao.

About the author

Alex Sonna