Featured Kitaifa

ZUBEIR ACHAGULIWA TENA KUONGOZA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR

Written by Alex Sonna

ZANZIBAR:

Zubeir Ali Maulid amechaguliwa tena kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa kipindi cha tatu mfululizo.

Uchaguzi huo umefanyika leo Alhamisi, Novemba 6, 2025, katika mkutano wa kwanza wa Baraza la 11 la Wawakilishi Zanzibar, na unamfanya Zubeir kuendeleza wadhifa huo aliouanza tangu mwaka 2015.

Spika Zubeir, ambaye anatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameshinda kwa kura 53 kati ya kura 68 zilizopigwa, sawa na asilimia 94.6, na kuwabwaga wagombea wenzake watatu — Chausiku Khatib Mohamed (NLD) aliyepata kura 3, Naima Salum Hamad (UDP), na Suleiman Ali Khamis (ADC) ambao hawakupata kura hata moja.

Kabla ya upigaji kura, Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Msellem, aliwaelekeza wagombea wote wanne kujieleza kwa dakika tano kila mmoja ili kuomba ridhaa ya wajumbe.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu Raya alisema jumla ya wajumbe 68 walishiriki katika mchakato huo wa kupiga kura ndani ya ukumbi wa Baraza hilo.

About the author

Alex Sonna