Featured Kitaifa

JESHI LA ZIMAMOTO DODOMA LAPOKEA MITAMBO NA VIFAA VYA KISASA

Written by Alex Sonna
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Ili kuongeza ufanisi katika kukabiliana na majanga ya moto na kuimarisha huduma za uokoaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoani Dodoma limepatiwa mitambo na vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Shilingi bilioni 52 kutoka Serikalini.

Makabidhiano ya vifaa hivyo yamefanyika leo, Jumatatu Oktoba 26, 2025, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

Mitambo hiyo inajumuisha jumla ya magari nane ya kisasa, yakiwemo mtambo mmoja wa kuzima moto, mtambo wa maokozi nchi kavu, magari mawili ya kubebea majeruhi, gari moja la kusimamia operesheni, gari moja la kubeba maji ya dharura, na gari maalum lenye katakana inayotembea.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa Senyamule ameipongeza serikali kwa kuendelea kuimarisha uwezo wa jeshi hilo, huku akitoa rai kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto kwa kukata bima na kutumia vifaa vya umeme kwa usalama.

“Ni muhimu wananchi kuzingatia matumizi salama ya vifaa vya umeme na pia kukata bima za majengo yao ili kupunguza athari pindi majanga yanapotokea,” amesema Senyamule.

Aidha, amewahimiza wakazi wa Dodoma kuendelea kujenga majengo makubwa ikiwemo maghorofa, akieleza kuwa mitambo hiyo ya kisasa ina uwezo wa kufanya shughuli za uokoaji hadi kwenye jengo lenye ghorofa 11.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Mwandamizi Rehema Menda, amesema ujio wa magari na mitambo hiyo utaleta mapinduzi makubwa katika utoaji wa huduma za uokoaji na uzimaji moto.

“Tangu Januari mwaka huu, tumeshuhudia matukio 256 ya majanga ikiwemo matukio 176 ya moto na maokozi 76. Ujio wa vifaa hivi utatusaidia kufika kwa haraka na kupunguza madhara kwa waathiriwa,” amesema Menda.

Ameongeza kuwa awali jeshi hilo lilikuwa likikabiliwa na changamoto ya upungufu wa vifaa, jambo lililokuwa likisababisha kuchelewa kufika kwenye baadhi ya maeneo ya dharura.

“Wakati mwingine tunapokea simu nyingi za maombi ya msaada lakini tunashindwa kufika kwa wakati kutokana na uhaba wa magari. Hivyo ujio huu ni faraja kubwa kwetu,” alisisitiza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Alhaji Shekimweri, amewataka wananchi kushirikisha wataalamu wa halmashauri katika ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha kunakuwa na mpangilio mzuri utakaorahisisha huduma za uokoaji.

“Ni muhimu miradi ya ujenzi ikahusisha wataalamu wa manispaa ili kupatiwa ushauri sahihi. Hii itarahisisha shughuli za uokoaji na kuzuia madhara wakati wa majanga,” amesema Shekimweri.

Ujio wa mitambo hiyo ya kisasa unatarajiwa kuongeza ufanisi mkubwa katika shughuli za zimamoto na uokoaji mkoani Dodoma, hususan kutokana na ongezeko la majengo makubwa na shughuli za maendeleo katika makao makuu ya nchi.

About the author

Alex Sonna