Featured Kitaifa

SERIKALI YAJIPANGA KUBADILISHA SEKTA YA ELIMU KUKABILI MAHITAJI YA UCHUMI WA KISASA

Written by Alex Sonna

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi,akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Pamoja wa Mapitio ya Sekta ya Elimu (AJESR) wa mwaka 2024/25.


Na.Alex Sonna-, Dodoma

SERIKALI imesisitiza dhamira yake ya kuibadilisha sekta ya elimu ili iendane na mahitaji ya uchumi wa dunia unaobadilika kwa kasi na unaoendeshwa na teknolojia, huku ikihakikisha elimu jumuishi, yenye usawa na ubora kwa wote.

Akizungumza  jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Pamoja wa Mapitio ya Sekta ya Elimu (AJESR) wa mwaka 2024/25, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, alisema serikali imejipanga kuhakikisha mfumo wa elimu unaendana na mikakati ya maendeleo ya taifa, ikiwemo ajenda ya uendelezaji wa viwanda na ubunifu chini ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050.

“Huu ni miongoni mwa mikutano muhimu zaidi katika mfumo wetu wa elimu kwani unatoa jukwaa rasmi la majadiliano ya sekta nzima, uwajibikaji wa pamoja na kupanga kwa kuzingatia ushahidi,” alisema Profesa Mushi.

Mkutano huo, unaobeba kaulimbiu “Kubadilisha Elimu kwa Maendeleo Endelevu,” unawakutanisha wadau kutoka serikalini, asasi za kiraia, taasisi za dini, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa sekta ya elimu, kutambua changamoto, na kuweka vipaumbele vya mwaka unaofuata.

Profesa Mushi alisema serikali inaendelea kuangalia elimu kama uwekezaji katika rasilimali watu, badala ya kuiangalia kama huduma ya kijamii pekee, akibainisha kuwa nchi inajenga nguvu kazi yenye ujuzi na weledi wa kuendesha ubunifu na kuongeza tija.

“Dunia inabadilika kwa kasi, teknolojia inachukua nafasi kubwa, hivyo tunahitaji rasilimali watu waliobobea watakaoweza kwenda sambamba na maendeleo hayo ya kiteknolojia,” alisisitiza Prof. Mushi.

Alipongeza wadau wa elimu kwa mafanikio yaliyopatikana katika mwaka 2024/25, ikiwemo kuongezeka kwa upatikanaji wa elimu, maboresho ya mafunzo kwa walimu, mageuzi ya mitaala na kuboreshwa kwa mifumo ya tathmini ya wanafunzi.

Amesema kupitia AJESR, Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu na kifedha ambao umechangia kuunganisha sayansi, teknolojia na ubunifu katika mfumo wa elimu, hatua inayoiweka nchi katika nafasi nzuri ya kukabiliana na mahitaji ya uchumi wa karne ya 21.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Bw. Atupele Mwambene, alisema elimu ni nguzo kuu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 na msingi wa maendeleo ya rasilimali watu nchini.

“Rasilimali watu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote. Ukuaji wa uchumi unaotegemewa unatokana na maandalizi bora ya rasilimali watu,” alisema Bw. Mwambene, huku akisisitiza kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaendelea kusaidia shule katika kutekeleza mageuzi ya elimu ipasavyo.

Kwa niaba ya washirika wa maendeleo, Mkuu wa Ofisi ya Tume ya Uingereza nchini Tanzania, Bi. Godfrida Magubo, aliipongeza serikali kwa kipaumbele inachokipa elimu chini ya Dira ya 2050, akisema kuwa ukuaji jumuishi hautowezekana bila wananchi walioelimika vizuri.

Bi. Magubo alishauri serikali kuharakisha maandalizi kwa ajili ya mwaka 2027, ambapo takribani wanafunzi milioni 5.1 watajiunga na shule za sekondari za chini, kutokana na kupunguzwa kwa muda wa elimu ya msingi kutoka miaka saba hadi sita.

Ametoa wito wa kuongeza madarasa, walimu na vifaa vya kujifunzia, huku akihimiza ushirikiano zaidi na sekta binafsi pamoja na taasisi za dini katika kupata rasilimali za kufanikisha mabadiliko hayo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Simon Nanyaro, aliipongeza serikali kwa kuwekeza katika mafunzo ya walimu, akibainisha kuwa walimu 70,657 wa shule za msingi na 67,254 wa sekondari wamepatiwa mafunzo, ongezeko kubwa ikilinganishwa na walimu 1,250 waliokuwa wamefunzwa hapo awali.

“Tunapopitia utendaji wa elimu kwa mwaka 2024/25, tunasherehekea mafanikio na kupanga njia ya kwenda mbele. Tuitumie hekima na utaalamu wetu wa pamoja kuinua zaidi ubora na usawa wa elimu nchini,” alisema Bw. Nanyaro.

About the author

Alex Sonna