Featured Kitaifa

SERIKALI IMEONESHA DHAMIRA YA DHATI KULINDA MAISHA YETU DHIDI YA MAMBA – WANANCHI MARA

Written by mzalendo

              Na Mwandishi wetu, Mara

Wananchi wa wilaya ya Bunda mkoani Mara wamekiri kuiona dhamira ya dhati ya Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA ya kutatua migongano baina ya wanyamapori na binadamu Kwa kuongeza Idadi ya vizimba, hatua inayotajwa kupunguza athari Kwa wananchi hao.

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 22, 2025 wakati wa ziara ya kukagua vizimba hivyo ikienda sambamba na utoaji elimu ya kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyampori aina ya mamba na viboko iliyofanywa na maofisa wa TAWA mkoani humo.

Miongoni mwa wananchi aliyewahi kujeruhiwa na mamba, Kurwa Ryoba mkazi wa Kijiji cha Buzimbwe ameishukuru Serikali Kwa hatua hiyo ya kuongeza Idadi ya vizimba akisema vizimba hivyo ni suluhisho muhimu katika kuokoa maisha ya wananchi, huku akiwasisitiza wananchi wenzake kutopuuzia kutumia vizimba hivyo ili wasije wakapata madhara aliyoyapata yeye.

“Naishukuru sana Serikali kutujengea kizimba hiki, maana kabla hakijajengwa watu walipata madhara akiwemo ndugu yangu” alisema Ryoba.

“Wananchi wenzangu, kizimba hiki kimejengwa hapa lakini naona wengine wanadharau kukitumia, wakipata madhara wanaanza kuilaumu Serikali. Mimi nawashauri wajifunze kutoka kwangu, wachukue tahadhali watumie vizimba, Serikali imefanya maneno mazuri kutujengea vizimba” ameongeza mkazi huyo wa Kijiji cha Buzimbwe.

Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema Kufuatia changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu nchini hususani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Serikali kupitia TAWA katika bajeti ya Mwaka 2024/25 ilitenga zaidi ya shillingi million 210 Kwa ajili ya kuongeza Idadi ya vizimba vipya Saba (7) ambapo Kwa wilaya ya Bunda pekee vizimba vinne tayari vimekamilika na vinaendelea kutumiwa na wananchi.

Aidha ametoa rai Kwa wananchi hao kuwa na matumizi sahihi ya vizimba hivyo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanavilinda ili viendelee kuwa msaada kwao.

“Hatujisikii furaha kusikia wananchi wanapata madhara ya wanyamapori hawa, hivyo ni muhimu mzingatie matumizi sahihi ya vizimba hivi Kwa ajili ya usalama zaidi ili kujiepusha athari hizo. Vilevile Serikali imetumia gharama kubwa kuvijenga, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuvilinda ili viendelee kuwa msaada ” alisema Maganja.

Naye Afisa Uhifadhi Kutoka Kanda ya Ziwa, Sato Masinde amewashauri viongozi wa vijiji kuunda Sheria ndogo ndogo ikiwa ni hatua muhimu ya kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa ipasavyo na kuendelea kuwanufaisha wananchi hao.

About the author

mzalendo