Featured Kitaifa

WATOTO 124,498 RUKWA WASAJILIWA NA RITA

Written by mzalendoeditor

 Baadhi ya viongozi wa dini na wa mila wa mkoa wa Rukwa wakiwa kwenye kikao cha tathmini ya mpango wa usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya miaka mitano unaoratibiwa na RITA.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti jana akifungua kikao cha tathmini  amesema mkoa huo umefanikiwa kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 124,498 kupitia mpango wa usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya miaka mitano unaoratibiwa na RITA.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Charles Salyeem akitoa taarifa ya mpango wa usajili wa watoto chini ya miaka mitano jana mjini Sumbawanga ambapo amesema tayari watoto milioni 7.5 katika mikoa 22 ya Tanzania Bara wamesajiliwa na kupatiwa veti vya kuzaliwa tangu mpango huo ulipozinduliwa Novemba 2021.

Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Denis Bandisa akizungumza jana kwenye kikao cha tathmini ya mpango wa usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano kikao kilichofanyika mjini Sumbawanga na kushirikisha viongozi wa mkoa, wilaya na taasisi za umma na binafsi.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa)

………………………………………..

Na. OMM Rukwa

Mkoa wa Rukwa umefanikiwa kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto 124,498 chini ya mpango wa Usajili wa watoto walio na umri chini ya miaka mitano unaoratibiwa na Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) ulioanza Novemba mwaka 2021 .

Mafanikio hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti  jana (16 Mei, 2022) wakati akifungua kikao cha tathmini kuhusu utekelezaji wa mpango huo kilichofanyika mjini Sumbawanga.

“Mkoa wetu katika mpango huu tumesajili watoto 124,498 sawa na asilimia 47.7 ya lengo la kusajili watoto 263,239. Ikumbukwe kwamba kabla ya kuanza mpango huu hapo Novemba 2021 tulikuwa na asilimia 5.8 hivyo tumeongeza usajili wa watoto kwa asilimia 41.9 “alisema Mkirikiti.

Mkirikiti alibainisha changamoto  kuwa cheti cha kuzaliwa kinatolewa kwa watu waliozaliwa katika ardhi ya Tanzania pekee na kutokana na mkoa wa Rukwa kuwa na mwingiliano mkubwa wa wananchi wa nchi jirani imekuwa ngumu kuwatambua wanaostahili kusajiliwa na kupata nyaraka.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito wananchi kuendelea kujitokeza kusajili watoto wao chini miaka mitano kwa kuwa cheti kinatolewa bure na hakuna fedha yoyote mwananchi atakayochangia.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Charles Salyeem alisema Mpango huo umeleta maboresho makubwa katika mfumo wa usajili wa vizazi na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto kwani sasa huduma hiyo inapatikana katika Ofisi za Watendaji Kata na Vituo vya Tiba kote mkoani Rukwa.

Salyeem alisema pia RITA kupitia mpango huo (Under 5 Birth Registration Iniative-U5BRI) ulioanza Novemba22, 2021 umefanikiwa kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto Milioni 7.5 katika mikoa 22 ya Tanzania Bara ambapo kiwango cha usajili kimeongezeka toka asilimia 13 hadi kufikia asilimia 65.

Alitaja changamoto ya wazazi wengi kutokuwa na Kitambulisho cha Taifa kuwa ni kikwazo cha watoto wengi kufikiwa, hata hivyo RITA kwa kushirikiana na Wakala wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) wanaendelea kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo.

Mpango huu unatekelezwa na RITA kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF), Serikali ya Canada, NIDA, Uhamiaji, OR- Tamisemi na kampuni ya Simu za Mikononi ya TIGO.

Kikao hicho cha tathmini kimehudhuriwa na wakuu wa wilaya za Sumbawanga, Nkasi na Kalambo, wajumbe wa kamati ya usalama mkoa, wakurugenzi wa halmashauri, Makatibu Tawala wilaya, viongozi wa dini na mila , Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Waganga wakuu wa Wilaya zote za mkoa wa Rukwa. 

Mpango huu kwa mikoa ya Rukwa na Katavi ulizinduliwa kwa mara ya kwanza Novemba 25 mwaka 2021 na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi mkoani Katavi.

About the author

mzalendoeditor