Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema amani inayofurahiwa na Watanzania leo haijaja kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya misingi imara ya uongozi, mshikamano na maadili ya kitaifa yaliyowekwa na waasisi wa taifa na kuendelezwa na viongozi wa kizazi cha sasa.
Akizungumza Oktoba 18,2025 wakati wa mazoezi ya kuhamasisha amani jijini Dodoma, Senyamule amewapongeza waasisi wa taifa kwa kuijenga Tanzania katika msingi wa upendo na umoja, akisema jukumu la kizazi cha sasa ni kuendeleza na kulinda amani hiyo kwa vitendo.
“Amani hii tumeirithi kwa gharama kubwa, hatupaswi kuichezea,lazima tuiheshimu na kuilinda kwa uchungu,” amesema kwa msisitizo.
Amefafanua kuwa Tanzania imejipambanua kama kisiwa cha amani barani Afrika, tofauti na mataifa mengi yanayokabiliwa na migogoro.
Hata hivyo, amewaonya wananchi kuwa amani hiyo inaweza kupotea endapo haitalindwa.
“Amani hupotea isipolindwa,ukosefu wa amani hujenga chuki, huondoa mapatano, hupoteza haki na kuchelewesha maendeleo ya watu,” amesema.
Senyamule amewataka wananchi wote wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla kutoruhusu vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani, iwe majumbani, mitaani au katika majukwaa ya kisiasa.
Amesisitiza kuwa kulinda amani kunahitaji utayari wa hali ya juu na uwajibikaji wa kila mmoja. “Tukate kufanya vitendo viovu. Kila mmoja awe mlinzi wa amani, bila kujali anazungumza nini mwingine kuhusu nchi yetu,” aliongeza.
Akiwaomba viongozi wa dini kuendelea kuwa nguzo muhimu ya maadili, Senyamule amesema sauti za viongozi hao zina nafasi kubwa katika kudumisha utulivu na mshikamano wa taifa.
“Viongozi wa dini muendelee kukemea uovu, kusisitiza amani na kuiishi kwa vitendo,” amesema huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya dini na serikali.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesema wananchi wa Dodoma wameonesha ukomavu wa kisiasa kwa kuamua kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya uchaguzi kwa njia ya amani.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Dodoma, Chifu Bilingi Yassir Ally wa Nne, amesema utulivu na mshikamano ni urithi ulioachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na ni wajibu wa kila Mtanzania kuuenzi kwa vitendo.
“Amani ndiyo nguzo ya maendeleo, na sisi kama Machifu tuna wajibu wa kuhakikisha hakuna anayeichezea tunu hii,Ole wao watakaothubutu kuleta vurugu au kujaribu kuivuruga Dodoma, maana tutasimama imara kuilinda nchi yetu,” amesema Chifu Bilingi kwa msisitizo.
Ameongeza kuwa ni haki ya kila raia kupiga kura kwa utulivu, akieleza kuwa kushiriki uchaguzi kwa amani ni heshima kwa Taifa na uthibitisho wa ustaarabu wa kisiasa wa Watanzania.
“Si dhambi kumuombea kura Chifu mwenzangu Hangaya anayeonyesha maono ya kuendeleza amani,tunachotaka ni nchi iendelee kuwa tulivu na yenye upendo,” ameongeza Chifu huyo.
Aidha amewatoa hofu wananchi wa Mkoa wa Dodoma kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu, akibainisha kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na usalama.
“Uchaguzi wa amani unawezekana, na tunaona Serikali yetu mejipanga kuhakikisha kila mtu anakuwa salama siku hiyo,” amesema
Naye Mwenyekiti wa Chama cha waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma, Chacha Marwa ameeleza kuwa vijana wameamua kuunga mkono juhudi za Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu wanaamini amani ndiyo msingi wa maendeleo na maisha bora.
“Ukiheshimu kura, unalinda sauti yako,Ukilinda amani, unalinda maisha yako,kamwe tusitumie mikono yetu kuharibu amani,” amesema Chacha.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Wafanyabiashara Wadogo mkoa wa Dodoma (Machinga), Hawa Maulidi Athumani, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuienzi amani na kudumisha upendo, akibainisha kuwa biashara ndogo ndogo hukua katika mazingira tulivu pekee.
“Biashara zetu hufanikiwa pale ambapo kuna utulivu,ni jukumu letu sote kulinda hali hii ili mambo yetu yaende kwa usalama,” amesema.
Amesema wao kama wafanyabiashara wanawajibika pia kama walezi wa jamii wana jukumu kubwa la kuhubiri amani majumbani, makazini na katika mikusanyiko yote.
“Kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuwa balozi wa amani,tukihifadhi amani, tunahifadhi vizazi vyetu,” amesema Madidi.
Dodoma imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika kudumisha amani na utulivu, huku viongozi wa Serikali, jamii na makundi mbalimbali wakiapa kushirikiana kuhakikisha uchaguzi wa Oktoba 29 unakuwa wa amani, huru na wa haki.