Featured Kitaifa

UJENZI WA DARAJA LA 6 KWA UREFU TANZANIA LA PANGANI WAFIKIA ASILIMIA 74.3

Written by Alex Sonna

 

Ujenzi wa Daraja la Pangani lenye urefu wa mita 525 na Barabara unganishi na mchepuko zenye urefu wa Kilomita 25 hadi tarehe 30 Septemba 2025 umefikia asilimia 74.3 na kazi ambazo zimefanyika ni pamoja wa Ujenzi wa kuta 2 unganishi za Daraja (Abutments) na nguzo 8 za Kati (Pier) ambapo jumla ya shilingi Bilioni 45.6 zimeshalipwa kwa mkandarasi.

Ujenzi wa daraja hilo ni dhamira kuu ya Serikali kuufungua na kuunganisha Mkoa wa Tanga na ushoroba wa Ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki unaoanzia Malindi – Mombasa – Lunga Lunga/Horohoro – Tanga – Pangani – Bagamoyo (Makurunge) wenye urefu wa kilomita 454.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga Mhandisi Msama Msama wakati alipokagua ujenzi wa mradi huo leo tarehe 14 Octoba 2025 na kuongeza kuwa Daraja hilo likikamilika litakuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi ikiwa ni pamoja na kupunguza muda wa usafiri, urahisishaji wa kufanya biashara na kuwezesha wananchi kuchangamana kwa urahisi, kuwezesha kufikika kwa urahisi kwenye vivutio vya utalii, kuwa kiungo kizuri kati ya bandari za Dar es salaam, Tanga na Mombasa na kuchochea uchumi wa Buluu.

Eng Msama amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kwanza ya Tanga – Pangani Kilomita 50 unafadhiliwa kwa asilimia 100 na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Ujenzi na kutekelezwa na TANROADS na Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni CHICO kutoka China umefikia asilimia 75 ya utekelezaji. Sehemu ya pili ya ujenzi wa mradi huo ni Daraja la Pangani na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 25.6 zinajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sehemu ya tatu ni ujenzi wa barabara ya Tungamaa – Mkwaja – Mkange ambayo imefikia asilimia 53 ya ujenzi na ina urefu wa Kilomita 95.2 ambapo itagharimu Shilingi Bilioni 94.538

Hali kadhalika, ameeleza kuwa barabara hiyo itawezesha wananchi kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo hususani Mihogo, nazi na mwani na hivyo itarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji hadi katika masoko mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Tanga.

Vilevile, Mhandisi Msama ameeleza kuwa TANROADS Mkoa wa Tanga inaendela na utekelezaji wa ujenzi wa miradi 3 ya dharura katika mkoa wa Tanga iliyotokana na kadhia iliyojitokeza ya mvua za El Nino na Kimbunga Hidaya ambayo itatumia jumla ya shilingi Bilioni 11.27 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo ya dharura.

Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na Daraja la Msangazi lenye urefu wa mita 30 lililopo katika barabara ya Amani – Muheza Kilomita 2 kutoka barabara kuu ya Tanga – Segera linalojengwa kwa shilingi Bilioni 4, mradi mwingine ni Boksi Caravati la Bwiko lililopo kilomita 2 kutoka kijiji cha Bwiko katika barabara ya Same – Segera kwenye barabara kuu ya Arusha – Moshi – Dar es salaam lenye urefu wa Mita 16.5 na barabara unganishi zenye urefu wa Mita 630 mradi utakaojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 3 pamoja na mradi wa ujenzi wa Daraja la Sagasa lenye urefu wa mita 39 katika barabara ya Kwaluguru – Kiberashi litakalojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 4.1

About the author

Alex Sonna