Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema kuwa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imefanya kazi kubwa ya kuboresha mazingira ya walimu, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule ambayo imeongeza ufanisi wa ufundishaji na ujifunzaji.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani Oktoba 03, 2025 Wilaya ya Bukombe, Mkoani Geita, Prof. Nombo ameeleza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na majukumu ya kutunga na kusimamia utekelezaji wa sera ya elimu, inasimamia pia maendeleo ya elimu msingi, mafunzo ya ualimu tarajali, na mafunzo ya walimu kazini jambo linaloonesha uzito wa nafasi ya walimu katika nyanja zote za elimu.
Prof. Nombo amesisitiza kuwa juhudi hizo zimewapa walimu uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, na kuongeza umahiri katika kufundisha na kujifunza.
Aidha, ameongeza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na wadau mbalimbali, imeandaa miongozo ya mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA), inayotekelezwa katika shule na vituo vya walimu ili kuwawezesha walimu kujiendeleza kitaaluma, kuimarisha mbinu za ufundishaji, na kuinua viwango vya ufaulu wa wanafunzi.
Prof. Nombo amebainisha kuwa Mpango wa MEWAKA umetambuliwa na Mkurugenzi wa Elimu wa Benki ya Dunia kama mfano bora wa kutambua na kuthamini juhudi za walimu ambapo kupitia mpango huo, walimu wamepata mafunzo katika maeneo ya utekelezaji wa mitaala, ufundishaji wa masomo ya sayansi, hisabati, TEHAMA, tathmini, ushauri na unasihi, usawa wa kijinsia, ujumuishi, na utunzaji wa mazingira.
Akizungumzia maslahi ya walimu, Prof. Nombo amesema kuwa kutokana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014/2023, Wizara imeandaa mkakati wa kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya walimu katika ngazi zote za elimu, na Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji ili kuwahimiza walimu kuendelea kutoa mchango katika sekta ya elimu.
Katibu Mkuu huyo alihitimisha kwa kusema kuwa kwa kushirikiana na wadau kama Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Wizara imeanzisha programu ya Leaders in Teaching, inayolenga kuimarisha mbinu za ufundishaji, kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa walimu, na kuwatia motisha ili kuboresha elimu nchini.