Featured Kitaifa

MALEZI BORA YA WATOTO NI MSINGI WA MAENDELEO YA TAIFA – KITIKU

Written by Alex Sonna

Na Jackline Minja – WMJJWM
Dodoma

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Sebastian Kitiku, amewataka wazazi na walezi kote nchini kuhakikisha wanawalinda na kuwalea watoto katika misingi bora ya malezi ili kujenga kizazi chenye afya njema na kitakacholeta maendeleo ya taifa.

Ameyasema hayo Oktoba 1, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na wanakikundi cha Tusaidiane Bondeni Ihumwa wakati wa majaribio ya kitini cha Malezi ya makundi.

Kitiku amesema kitini hicho ni nyenzo muhimu ya kuwaongoza wazazi na walezi katika kusimamia malezi chanya ya watoto ikiwa lengo la Wizara ni kuhakikisha kila mtoto analelewa katika mazingira bora yanayojali afya ya mwili, akili na ustawi wa kihisia.

“Wazazi na walezi mnapaswa kutambua kuwa malezi mnayowapa watoto leo ndiyo yatakayounda jamii ya kesho, maana kwa sasa tuna changamoto katika kuwalea watoto wetu, namna tulivyolelewa sisi ni tofauti na malezi ya sasa hivi maana hata mimi nikijiuliza na ninyi pia mnajiuliza hivi tunatengeneza taifa la namna gani! Lakini mlivyoondoka nyumbani na kuja hapa kuna baadhi ya watoto mmewaacha huko sasa tukasema kupitia vikundi vya namna hii vikikutana angalau wawe wanazungumza kuhusu malezi ya watoto” amesema Kitiku.

Aidha Mkurugenzi Kitiku amesema jukumu la malezi si la Serikali pekee bali ni la kila mzazi, mlezi na jamii kwa ujumla, na kusisitiza kuwa ushirikiano wa wadau wote ni nguzo ya mafanikio katika kujenga taifa imara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo na Mtoto, Asha Vuai amesema kuwa malezi bora ni msingi wa kizazi chenye uzalendo na heshima kwa taifa, hivyo kitini hicho kitawezesha kwenye vikundi kupata muongozo mzuri wa namna ya kuwalea watoto, kuwapatia mwongozo na kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kuharibu ndoto zao.

Nao baadhi ya wanakikundi cha Tusaidiane Bondeni Ihumwa wameipongeza Serikali kwa kuwaletea elimu hiyo ambayo itawasaidia kulea watoto wenye afya njema ya mwili na akili, ambao watakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi hivyo elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu namna bora ya kumlea mtoto, ikiwemo umuhimu wa mawasiliano ya karibu kati ya mzazi na mtoto, ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili pamoja na kuwajengea watoto maadili na nidhamu ya kujithamini.

“Tunashukuru Serikali kupitia Wizara kwa kuona umuhimu wa malezi na kuwekeza kwenye elimu hii. Imetufungua macho na sasa tupo tayari kushirikisha wenzetu kwenye vikundi vingine ili kila mtoto apate malezi bora yatakayomsaidia kufanikisha ndoto zake,” alisema mmoja wa wanachama wa kikundi hicho.

Kwa mujibu wa Wizara mikakati ya malezi chanya ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za Serikali katika kujenga familia imara na kuimarisha jamii, ikiwemo kupitia Sera za Ustawi wa Mtoto, Kampeni za Malezi Bora na Programu za Elimu endelevu zinazoshirikisha wadau wa sekta binafsi na mashirika ya kiraia.

Majaribio hayo yalitanguliwa na mafunzo ya siku tatu yaliyoshirikisha Mashirika binafsi, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii na vikundi vya malezi. Washiriki hao waliandaliwa ili kuwa mabalozi wa elimu ya malezi chanya watakaoifikisha kwa vikundi na jamii mbalimbali nchini.

About the author

Alex Sonna