Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed,akizungumza wakati akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee iliyofanyika wilayani Songea, mkoani Ruvuma.
Na Abdala Sifi – WMJJWM -Ruvuma
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed amesema jamii inapaswa kuwaenzi na kuwalinda wazee kwani wazee ni urithi na alama kwa Taifa.
Brigedia Jenerali Abbas amesema hayo tarehe 1 Oktoba, 2025 wakati akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee iliyofanyika wilayani Songea, mkoani Ruvuma.
Ameongeza kwamba wazee ndiyo msingi wa amani na utulivu wa Nchi, hivyo ni muhimu jamii kuzingatia vyema haki ustawi wao kwa maendeleo endelevu.
Aidha ametoa rai kwa wazee kushiriki uchaguzi mkuu ujao ili kupata viongozi watakaoendelea kutetea na kuweka mazingira rafiki kwa kuzingatia sheria na sera zilizopo zinazosimamia huduma kwa wazee nchini.
” Niipongeza na kuishukuru Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuandaa maadhimisho hayo katika Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.” amesisitiza Brigedia Jenerali Abbas
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema wazee ni walinzi, walezi na washauri wa mila na desturi chanya katika jamii hivyo ni muhimu kila mtu kuhakikisha anawatunza na kuwaenzi kwa ustawi na maendeleo ya Taifa.
Wakili Mpanju pia ametoa wito kwa vijana kujenga utamaduni wa kuwatembelea wazee wao kwa lengo la kujifunza maadili mema na urithi wa mila chanya kwa sababu ndizo msingi wa jamii inayoheshimu utamaduni wake.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa Lameck Sendo amesema Wazee watashiriki kushiriki uchaguzi Mkuu ili kupata viongozi watakaosimamia haki na stahiki zao katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za kijamii.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “ Wazee Tushiriki Uchaguzi Mkuu Kwa Ustawi wa Jamii Yetu” ikiwa na lengo la kuhamasisha kila mtu kutimiza haki yake ya msingi na kikatiba kwa kushiriki katika uchaguzi wa viongozi.