Featured Kitaifa

PPRA YAWANOA WATUMISHI OFISI YA MHASIBU MKUU WA SERIKALI KUFANYA MALIPO KUPITIA NeST

Written by Alex Sonna

MAMLAKA  ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imetoa wito kwa wahasibu wa Serikali kuunga mkono juhudi za kufanikisha malipo ya ununuzi wa umma kufanyika kupitia Mfumo wa NeST, baada ya mfumo huo kuunganishwa na mifumo ya malipo ya Serikali.

Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa PPRA, Wakili Paul Kadushi ametoa wito huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, alipofungua Mafunzo ya Usimamizi wa Mikataba na Utekelezaji wa Malipo kidigitali kupitia Mfumo wa NeST uliounganishwa na mifumo ya malipo ya Serikali, Septemba 29,2025, jijini Arusha.

“NeST imeunganishwa na mifumo zaidi ya 20 hadi sasa. Na hii imeonesha kuwa na tija kubwa kwakuwa mzabuni anapaswa kuhakikisha amekidhi vigezo vyote kwenye taasisi zinazompitisha. Pia, inasaidia kuhakikisha usahihi na ufanisi kwenye kila hatua ya mchakato wa ununuzi hadi yanapofanyika malipo,” amesema Kadushi.

Aliongeza kuwa kuunganishwa kwa mifumo ya taasisi za Serikali na Mfumo wa NeST kumetoa faida kwa taasisi zote za umma pamoja na wazabuni, katika myororo wa kuwaletea wananchi maendeleo.

Wakili Kadushi amewasihi watumishi hao kufuatilia mafunzo kwa umakini zaidi ili kusaidia kufanikisha utekelezaji wa nia ya Serikali ya kuunganisha mifumo ya malipo na Mfumo wa NeST.

Awali, Mhasibu Mkuu wa Serikali Msaidizi, Bi. Mary Kimambo alipongeza PPRA kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwataka washiriki kuhakikisha wanapata uelewa wa kutosha ili watekeleze kwa ufanisi majukumu yao na kuongeza tija kwenye sekta ya ununuzi wa umma.

About the author

Alex Sonna