Featured Kitaifa

SERIKALI NA BENKI YA DUNIA WAJADILI UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO INAYOFADHILIWA NA BENKI YA DUNIA

Written by Alex Sonna


Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza wakati wa Kikao kazi cha Country Portfolio Performance Review (CPPR) na ujumbe wa Benki ya Dunia kilichofanyika katika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bi. Milena Stefanova, akizungumza wakati wa Kikao kazi cha Country Portfolio Performance Review (CPPR) kilichofanyika katika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa jopo la wataalamu kutoka Benki ya Dunia ukiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bi. Milena Stefanova (wa tatu kulia) baada ya kumalizika kwa kikao kazi wengine ni wajumbe kutoka Benki hiyo na Wizara ya fedha, kilichofanyika katika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule akizungumza wakati wa Kikao kazi cha Country Portfolio Performance Review (CPPR) na ujumbe wa Benki ya Dunia kilichofanyika katika Ofisi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)

Na Chedaiwe Msuya, WF, Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ameihakikishia Benki ya Dunia kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana na Benki hiyo katika kutekeleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo kwa ufanisi, wakati na kwa viwango vinavyokusudiwa.

Dkt. Mwamba amesema hayo wakati wa kikao cha Country Portfolio Performance Review (CPPR) kinacholenga kubaini changamoto kuu za mfumo zinazokwamisha utekelezaji wa miradi na kuandaa mpango kazi wa pamoja wa kuzitatua kilichofanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.

kwa sasa, Serikali inaendelea kutekeleza jumla ya miradi 35 kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia, ikijumuisha miradi 29 ya kitaifa inayolenga sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi pamoja na miradi 6 ya kikanda inayotekelezwa, yote ikiwa na lengo la kuharakisha maendeleo endelevu ya taifa.

“Utekelezaji mzuri wa miradi hiyo unatarajiwa kuchangia katika kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi, sambamba na kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2050, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22–2025/26) pamoja na ZADEP 2021–2026” alisema Dkt. Mwamba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bi. Milena Stefanova ameishukuru Serikali kwa ushirikiano mzuri katika utekelezaji wa miradi.

“Benki ya Dunia inatambua na kushukuru ushirikiano unaotolewa na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa miradi, kuimarisha muundo wa pamoja wa kazi na kuhakikisha malengo ya maendeleo yanatimizwa kwa ufanisi” alisema Bi. Milena Stefanova.

Ushirikiano wa Serikali na Benki ya Dunia katika kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaweka msingi imara wa kuhakikisha miradi inakamilika kwa ufanisi, inaleta matokeo yanayotarajiwa kwa wananchi na kuchochea ustawi wa kijamii na kiuchumi wa Tanzania.

Aidha, pande mbili zilikubaliana kuandaa mpango kazi utakaofanyiwa mapitio kabla ya mikutano ya majira Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), itakayofanyika mwezi April mwaka 2026.

About the author

Alex Sonna