Na Abdala Sifi WMJJWM – Songea, Ruvuma
Mkuu wa Wilaya ya Songea Kapenjama Ndile amesema Wazee ni hazina ya Taifa hivyo jamii inatakiwa kuwaheshimu ,kuwalinda pamoja na kuwapatia haki zao za msingi.
Mhe. Ndile amesema hayo leo Septemba 30, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed wakati akifungua Kongamano kuelekea Siku ya Kimataifa ya Wazee itakalofanyika wilayani Songea mkoani Ruvuma.
“Wazee wetu ni hazina ya Taifa, hivyo kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha anawatunza Wazee kwa ajili ya ustawi wa maisha yao” amesema Ndile.
Pia ameeleza kuwa Tanzania inaungana na nchi nyingine kuadhimisha siku hiyo kwa lengo la kuhakikisha jamii inajengewa uelewa na kulinda maslahi na haki za wazee nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la Wazee Kitaifa Lameck Sendo amesema vijana wana wajibu wa kuwahudumia Wazee ikiwa ni pamoja na kuwapa malazi, chakula na mavazi, badala ya kuwatelekeza kwani vitendo hivyo ni ukatili dhidi yao.
Maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Wazee Tushiriki Uchaguzi kwa Ustawi wa Jamii Yetu” ambayo inalenga kuwahamasisha kushiriki kuwachagua viongozi bora watakaotetea maslahi na maendeleo yao.
Kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika tarehe 1, Oktoba 2025, Katika Ukumbi wa Songea Club ambapo zaidi ya washiriki elfu moja wanatarajiwa kuhudhuria.