KLABU ya Yanga SC ya Tanzania imetinga raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) baada ya ushindi wa jumla wa mabao 5-0 dhidi ya Williete SC kutoka nchini Angola.
Yanga SC ilianza kampeni yake kwa kishindo baada ya kushinda mabao 3-0 ugenini nchini Angola, kabla ya kumaliza kazi nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kwa ushindi wa mabao 2-0.
Katika mchezo wa marudiano uliofanyika leo Jumamosi, Septemba 27, 2025, mabao ya Yanga yalifungwa na Pacôme Zouzoua dakika ya 70 na bao la pili limefungwa na Aziz Andabwile dakika ya 86, na kuwanyanyua mashabiki kwa furaha ya kuendelea na safari ya Afrika.
Kwa ushindi huo, Yanga SC sasa itachuana na Silver Strikers ya Malawi katika raundi ya pili. Silver Strikers imelitinga hatua hiyo kwa faida ya bao la ugenini, baada ya kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Elgeco Plus ya Madagascar kwenye mchezo wa kwanza, kisha kulazimisha suluhu tasa ya 0-0 kwenye marudiano nyumbani Malawi.
Yanga SC italazimika kuwa makini zaidi hatua inayofuata, huku lengo lao kubwa likiwa ni kufika hatua ya makundi na kuendeleza historia katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.