Featured Kitaifa

WANANCHI WAIPONGEZA TARURA UJENZI WA MIUNDOMBINU

Written by Alex Sonna

Geita

Imeelezwa kwamba Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) hufanya usanifu wa kina wa barabara kabla ya ujenzi kuanza kutekelezwa.

Hayo yamebainishwa na Mhandisi wa miradi kutoka TARURA Faizer Mbange wakati akitoa elimu kwa umma kwa wananchi waliofika kwenye Maonesho ya Nane ya Madini Mkoani Geita.

Amesema kwamba barabara nyingi nchini zinazosimamiwa na Wakala kwa sasa zina hali nzuri kwani usanifu wa kina hufanyika pamoja na usimamizi madhubuti wakati wa utekelezaji wa mradi.

“Yote haya yanafanyika ili kuhakikisha thamani na viwango vya barabara vinafikiwa ili kukidhi mahitaji na kupata thamani ya fedha iliyokusudiwa katika ujenzi wa miundombinu”.

Naye, Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi kutoka TARURA Mkoa wa Geita Bw. Godfrey Vedasto amewataka wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya barabara zinazotengenezwa katika maeneo yao ili zidumu kwa muda mrefu.

Amesema serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara ikiwemo mitaro ya maji hivyo wananchi wanapaswa kuitunza na kutofanya shughuli kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara.

“Shughuli kwenye hifadhi ya barabara zikiwemo kutupa taka kwenye mitaro ya maji na hivyo msimu wa mvua mitaro hiyo hujaa uchafu na kusababisha mafuriko”.

Amesema mafuriko hayo husababisha maji kujaa kwenye makazi ya watu, kuharibu barabara na kusababisha milipuko ya magonjwa mbalimbali.

Pia Mkazi wa Geita Bw. Augustino Stephano ameipongeza TARURA kwa ujenzi wa barabara za mitaa pamoja na mitaro kwani hivi sasa barabara zinapitika kwa urahisi.

Amesema elimu waliyoipata kutoka kwa wataalam wa TARURA itawasaidia katika utunzaji wa mitaro na barabara na kutoa rai kwa wananchi wengine kutoa ushirikiano kwa Wakala huo kutunza miundombinu katika maeneo yao.

About the author

Alex Sonna