Na.Alex Sonna
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wameanza kampeni za kutetea ubingwa wao kwa kishindo baada ya kuichapa Pamba Jiji ya Mwanza mabao 3-0, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Yanga kuongoza bao 1-0, lililofungwa na kiungo mshambuliaji Lassine Kouma dakika ya 45+4 kwa kichwa, akimalizia kona iliyochongwa na Edmund John.
Baada ya mapumziko, kocha wa Yanga alifanya mabadiliko yaliyoongeza uhai kwenye safu ya ushambuliaji na dakika ya 63 Max Nzegeli akaongeza bao la pili, akimalizia pasi safi ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Kiungo Mshambuliaji Mudathir Yahya aliihakikishia Yanga pointi tatu muhimu baada ya kufunga bao la tatu dakika ya 90+2 kwa pasi ya Pacome Zouzoua.
Ligi hiyo itaendelea kesho ambapo wekundu wa Msimbazi, Simba SC, watakuwa wenyeji wa Fountain Gate ya Manyara kwenye uwanja huo wa Benjamin Mkapa.