Featured Kitaifa

MGOMBEA URAIS CHAUMMA AAHIDI SOKO LA KIMATAIFA KIBORILONI

Written by Alex Sonna

Na.Mwandishi Wetu-MOSHI:

MGOMBEA Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kujenga upya soko la kisasa la Kiboriloni, lenye hadhi ya kimataifa sawa na soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, endapo atachaguliwa kuwa Rais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.

Akihutubia  mkutano wa kampeni uliofanyika leo Jumamosi, Septemba 6, 2025 katika eneo la soko hilo, Mwalimu alisema hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya biashara, kuinua uchumi wa Moshi na kulinda mitaji ya wafanyabiashara wadogo ili waweze kukua.

Ameongeza kuwa soko hilo la kihistoria limekuwa likihudumia wateja kutoka mataifa jirani kama Kenya na Uganda, lakini kwa sasa limeachwa katika hali duni, hali inayowalazimu wafanyabiashara kufanya kazi kwenye mazingira magumu hususan nyakati za mvua.

“Ahadi ninayowapa watu wa Kilimanjaro, wa Kiboriloni na wafanyabiashara wote ni kwamba tutalijenga soko la kimataifa hapa. Watu kutoka Uganda na Kenya watakuja tena kununua bidhaa kama ilivyokuwa zamani,” alisema Mwalimu.

Amesisitiza kuwa kutokana na historia yake, soko hilo litajengwa kwa muundo wa kisasa na litakuwa na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara na wateja wa ndani na nje ya nchi.

About the author

Alex Sonna