Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mafinga katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama hicho mkoani Iringa tarehe 06 Septemba, 2025.
….
MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa itakayonufaika na ahadi ya CCM ya kujenga kongani za viwanda kwa vijana, kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na ufugaji nchini.
Akizungumza leo Jumamosi, Septemba 6, 2025, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Mafinga, Dkt. Samia amesema kuwa mpango huo utajumuisha pia kuendeleza viwanda vya usindikaji wa mazao ya misitu kutokana na wingi wa zao hilo katika mkoa huo.
“Iringa ina kilimo lakini pia ina uvunaji wa misitu. Moja ya kongani tulizoziwaza ni kongani ya mazao ya misitu. Tutafikiria wilaya gani kongani ya viwanda ikae ili vijana waongeze thamani ya mazao ya misitu na kutumia soko la ndani na la kimataifa kuuza bidhaa zao,” amesema Dkt. Samia.
Akiwahutubia maelfu ya wanachama wa CCM na wananchi wa Mafinga, Dkt. Samia amesisitiza kuwa serikali yake, endapo atapewa ridhaa ya kuendelea kuongoza, itaendeleza sera ya ruzuku kwenye sekta ya kilimo na ufugaji kwa kuendelea kutoa punguzo kwenye pembejeo, mbolea na mbegu pamoja na ruzuku ya chanjo kwa mifugo. Hatua hiyo inalenga kuongeza uzalishaji na kuimarisha sekta ya kilimo na mifugo nchini.
Aidha, kutokana na uzalishaji mkubwa wa mazao ya biashara katika mkoa wa Iringa, Dkt. Samia amebainisha kuwa serikali itaendelea kununua mahindi kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), sambamba na ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhia mazao hayo. Alisema hatua hiyo inalenga kuepusha upotevu na uharibifu wa mazao wakati wa msimu wa mavuno.