Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mafinga katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama hicho mkoani Iringa tarehe 06 Septemba, 2025.
Na Mwandishi Wetu, Iringa
MGOMBEA Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itakayoongozwa naye endapo atachaguliwa tena itaendeleza kasi ya maendeleo kwa nguvu zilezile katika sekta za elimu, afya, maji, umeme na miundombinu.
Akihutubia leo Jumamosi, Septemba 6, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mafinga, mkoani Iringa, Dkt. Samia amesema kuwa malengo makuu ni kuhakikisha kila Mtanzania anaguswa na huduma muhimu za kijamii na kiuchumi.
“Kasi ileile tuliyoenda nayo miaka mitano iliyopita ndiyo kasi tutakayoendelea nayo kwenye miaka mitano ijayo kwenye sekta ya elimu, afya, miundombinu, maji na umeme. Tunataka kila Mtanzania aguswe na vitu hivyo; awe na maji safi na salama, watoto wapate fursa ya kusoma kuanzia shule ya msingi, sekondari hadi vyuo. Pia tumejenga vyuo vya ufundi ili vijana wetu, hawa masela, wapate maeneo ya kuongeza ujuzi kwa kazi wanazozifanya,” amesema
Pia Dkt. Samia amesema kuwa serikali imeweka utaratibu wa kumsaidia kila Mtanzania asiye na uwezo, ili kila mmoja apate huduma za afya bila vikwazo. Aidha, alieleza kuwa upatikanaji wa umeme umeendelea kuwa kipaumbele, si kwa ajili ya kurahisisha shughuli za nyumbani na kiuchumi pekee, bali pia kwa kulinda usalama wa wananchi.
“Tunataka kila Mtanzania aone umeme utakaomsaidia kurahisisha kazi zake nyumbani, kufanya shughuli za kiuchumi na kulinda usalama wa maeneo yetu. Umeme ni usalama wa maeneo yetu,” ameongeza.
Aidha amegusia sekta ya miundombinu, amesema kuwa ujenzi wa barabara ni kichocheo kikubwa cha uchumi na serikali inajipanga kuendelea na miradi hiyo kwa kiwango kikubwa.
“Ujenzi wa miundombinu ni shughuli nyingine muhimu kwa uchumi wetu. Nimesikia kilio cha barabara, nataka niseme tunajipanga, jinsi tutakavyoweza na Mungu atakavyotuwezesha kuzijenga barabara za Tanzania yote. Hatutamaliza kwa miaka mitano ijayo, lakini kazi kubwa tutaifanya katika ujenzi wa barabara ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa kufika masokoni na watu kusafiri kwa haraka kwenda kufanya shughuli zao za kiuchumi, kijamii na kisiasa,” amesisitiza