Featured Kitaifa

MGOMBEA URAIS CUF AAHIDI ELIMU NA AFYA BURE

Written by Alex Sonna

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga

MGOMBEA wa urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito Gombo, ameahidi kuwa endapo atashinda Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, serikali yake itahakikisha elimu inatolewa bure kuanzia darasa la awali hadi chuo kikuu.

Akihutubia jana katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Stendi ya Mabasi ya Wilaya ya Shinyanga, Gombo alisema elimu ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya taifa, hivyo CUF ikipewa ridhaa ya kuongoza nchi, kila mtoto wa Kitanzania atapata nafasi sawa ya kusoma bila kikwazo cha ada.

“Tukipewa ridhaa, kila mtoto atasoma bure kuanzia darasa la awali hadi chuo kikuu. Elimu ndiyo msingi wa maendeleo, na serikali ya CUF itawekeza kwa nguvu zote kwenye sekta hii,” alisema Gombo

Pia  mgombea huyo aliahidi pia kufuta gharama za matibabu ili wananchi wote wapate huduma za afya bure, pamoja na kufuta kikokotoo cha pensheni ambacho, kwa mujibu wake, kimekuwa kikwazo kwa wastaafu kunufaika ipasavyo na mafao yao.

“Kikokotoo kimekuwa mwiba kwa wastaafu kushindwa kunufaika na mafao yao. Serikali ya CUF itakifuta mara moja ili wastaafu wapate heshima ya stahiki zao,” alisisitiza.

About the author

Alex Sonna