Featured Michezo

MULIRO AKABIDHI ASKARI WA KIKE BENDERA KWA NIABA YA IGP KWENDA SCOTLAND.

Written by Alex Sonna

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Jumanne Muliro amewakabidhi bendera ya Taifa askari wa kike kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura wanaokwenda katika mafunzo ya shirikisho la askari wa kike duniani (IAWP) nchini Scotland.

Amesema kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini anathamini mchango wa shirikisho hilo ambalo limesaidia sana kuleta chachu ya mabadiliko ya kiutendaji ndani ya Jeshi la Polisi tangu waanze kushiriki mafunzo hayo katika maeneo tofauti tofauti duniani.

Aidha Kamanda Muliro amesisitiza kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini amewataka maafisa na askari hao wanaokwenda nchini Scotland kuwa na nidhamu muda wote wa mafunzo kama ilivyo kauli mbiu ya Jeshi la Polisi Tanzania, nidhamu haki weledi na uadilifu.

Sambamba na hilo amewakumbusha kutumia vyema mafunzo hayo kujenga mtandao wa mawasiliano ambao utaliunganisha Jeshi la Polisi Tanzania na mataifa mengine duniani katika kupambana na uhalifu na kubadilishana uzoefu katika utendaji wa kazi za Polisi.

SACP Muliro amebainisha kuwa masomo ambayo yanakwenda kufundishwa ni Pamoja na Mkakati bunifu ya ulinzi kwa raia ili kuimarisha uaminifu katika ya vyombo vya sheria na jamii, kutumia sayansi data kuchunguza na kutabiri uhalifu, kupambana na ugaidi na uchunguzi wa kesi, biashara haramu ya binadamu na masomo mengine ambayo ni ya kimkakati katika kupambana na uhalifu.

Mwisho akaweka wazi kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini anategemea Maafisa na askari hao watumie fursa hiyo kutangaza uzuri wa Tanzania na vivutio vilivyopo nchini.

About the author

Alex Sonna