Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, akifunga Kikao Kazi cha Wataalam wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali na kuwataka kuimarisha utendaji wao kupitia mafunzo waliyoyapata kwa siku tano kwa wataalamu hao kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa, kuhusu Mfumo wa CBMS ulioboreshwa, yaliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Na. Hadija Saidi na Christina Dimosso, WF, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba amewapongeza Wataalam wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali kwa kushiriki kikamilifu katika mafunzo yaliyolenga kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za umma.
Pongezi hizo zimetolewa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Bw. Lusius Mwenda, wakati akifunga mafuzo ya siku tano ya Wataalamu hao kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa yaliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Bw. Mwenda alisema kuwa kikao hicho kimekuwa muhimu katika kuboresha usimamizi na ufuatiliaji wa fedha za umma na anaamini kila mshiriki amepata uelewa wa kutosha kumuwezesha kutekeleza bajeti ya fungu lake kwa ufanisi unaotarajiwa na Serikali.
“Katika Mafunzo haya mmepitishwa kwenye maelekezo yaliyotolewa kwenye Waraka wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2025/2026, maombi ya fedha za maendeleo, matumizi mengineyo na uhamisho ndani ya fungu kupitia Mfumo wa CBMS ulioboreshwa, tathmini ya namna ya kuboresha ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), maeneo ambayo ni muhimu katika utendaji kazi ikiwa yamezingatiwa ipasavyo”, alisema Bw. Mwenda.
Aliyataja maeneo mengi ambayo wataalamu hao wamepitishwa kuwa ni pamoja na kuhasibu bajeti ya Serikali, tathmini ya miradi inayotekelezwa kupitia mapango na bajeti ya Serikali, maudhui ya ndani ya utekelezaji wa mradi na matokeo yake kwenye Bajeti ya Serikali.
Vile vile wameangazia masuala ya Tafiti kuhusu vigezo vya ugawaji rasilimali fedha kwenye bajeti ya Serikali, matokeo ya utafiti wa matumizi ya Serikali kwenye sekta za Elimu, Afya na huduma za maji, tathmini ya UNICEF kuhusu uandaaji na utekelezaji wa bajeti ya Serikali na utawala bora katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali.
Bw. Mwenda alisema kuwa Waratibu wa kikao kazi hicho wamekusanya maoni mengi na maazimio, mambo ambayo ni muhimu katika utendaji kazi na kuandaa mwongozo, uandaaji mpango na bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/2027 ambayo ni nyenzo muhimu katika kutoa muelekeo wa bajeti ya Serikali na lakini pia maelekezo ya jinsi ya kuandaa mipango na bajeti ya mafungu yao.
Aidha amewahakikishia kuwa maoni yao yatafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuyazingatia wakati wa kuandaa mwongozo wa uandaaji wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/2027.
Ametoa rai kwa wataalamu watakaopenda kutoa maoni zaidi baada ya kikao kazi hicho kuendelea kutoa maoni kwa njia ya maandishi kwa kujaza dodoso kwa kuskani visimbo na kuwasilisha eneo husika.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, akifunga Kikao Kazi cha Wataalam wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali na kuwataka kuimarisha utendaji wao kupitia mafunzo waliyoyapata kwa siku tano kwa wataalamu hao kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali na Sekretarieti za Mikoa, kuhusu Mfumo wa CBMS ulioboreshwa, yaliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda (kushoto) na Kamishna Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Bajeti Wizara ya Fedha, Bw. Fundi Makama, wakiteta jambo wakati wa hafla ya kufunga kikao kazi cha Wataalam wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Baadhi ya Washiriki wa kikao cha mafunzo ya Mfumo wa Uandaaji na Usimamizi wa Bajeti (CBMS) ulioboreshwa, wakifuatilia mawasilisho mbalimbali yaliyotolewa katika kikao kazi cha Wataalamu wanaoandaa na kusimamia Bajeti ya Serikali kilichofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Dodoma)