Featured Kitaifa

DKT.SAMIA AAHIDI UJENZI WA BARABARA MOROGORO,AWATOA HOFU WANANCHI

Written by Alex Sonna

Na.Mwandishi Wetu-Morogoro 

MGOMBEA  urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Morogoro kuwa barabara za Bigwa – Mvua – Kisaki na Ubena Zomozi – Ngerengere zitajengwa kwa kiwango cha lami, ili kuondoa changamoto za miundombinu zinazowakabili kwa muda mrefu.

Akihutubia mkutano wa kampeni katika eneo la Ngerengere leo Agosti 29,2025 , Dk. Samia amesema serikali itahakikisha barabara hizo zinakamilika,huku akiwataka wananchi kuendelea kuwa na imani na Chama Cha Mapinduzi kwa kuwa kimekuwa kikitekeleza ahadi zake kwa vitendo.

“Nafahamu kuwa wakazi wengi wa Halmashauri hii ya Morogoro Vijijini ni wakulima wazuri. Ingawa kuna kilio cha ardhi, tumekichukua na tunakwenda kukifanyia kazi. Na kuhusu barabara, tunaijua changamoto yenu, na tutaiimaliza,” amesema Dk. Samia.

Amesema kwa sasa ujenzi wa barabara ya Ubena Zomozi hadi Ngerengere, yenye urefu wa kilomita 11.6, umefikia asilimia 24, na ameahidi kwamba serikali itahakikisha mradi huo unakamilika.

Aidha, amesema barabara ya Bigwa – Mvua – Kisaki nayo ni ya kimkakati na muhimu kwa wakazi wa eneo hilo, na kwamba amekuwa akisikiliza kilio cha wananchi kupitia viongozi wao, hususan mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Kusini-Mashariki, Hamis Taletale ‘Babu Tale’, ambaye mara kadhaa ameibua hoja ya uboreshaji wa miundombinu hiyo.

“Kila mara Babu Tale anaponiona hunikumbusha kuhusu barabara ya Bigwa – Kisaki. Mimi ni mkazi wa eneo hilo pia, nina mashamba kule. Hii barabara ni muhimu, na nitahakikisha inajengwa,” amesisitiza Dk. Samia.

Kauli hiyo imepokelewa kwa shangwe na wananchi waliokusanyika Ngerengere, huku wakionesha matumaini makubwa kwa utekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo.

      

Share this Article

About the author

Alex Sonna