Featured Kitaifa

MHANDISI SANGA AONGEZA MWEZI MMOJA KLINIKI YA ARDHI KIVULE KUONGEZA KASI YA UTOAJI HATI

Written by Alex Sonna

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga (katikati) akizungumza na wananchi Agosti 16, 2025 kwenye Kliniki ya Ardhi inayofanyika Kata ya Kivule Ilala Dar e salaam. Kulia ni Kamishna wa Ardhi Bw. Nathaniel Nhonge na kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Rehema Mwinuka.

Na Eleuteri Mangi, Dar es Salaam

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameongeza mwezi mmoja kwa watumishi wanaotoa huduma za ardhi kwenye Kliniki ya Ardhi inayofanyika Kata ya Kivule Ilala Dar e salaam kuanzia Agosti 18, 2025 ili kupunguza mzingo mkubwa kwa wananchi ambao hawana hati.

Mhandisi Sanga ametoa maekelezo hayo Agosti 16, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kivule ambao wanaendelea kupata huduma kwenye Kliniki hiyo.

“Tunatamani zoezi hili limalize changamoto zenu zote, kwa sababu tukimaliza changamoto zenu hapa hamtakuja ofisini, nawaagiza wasaidizi wangu, zoezi hili liendelee kwa muda wa mwezi mzima baada ya tarehe 18 Agosti 2025 ambayo ilipangwa ili kumaliza changamoto zenu za ardhi katika maeneo yenu” amesema Mhandisi Sanga.

Ili kuleta tija katika zoezi hilo, Mhandisi Sanga ameelekeza watumishi 10 waongezwe katika kliniki hiyo ambao watatoka maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza kasi ya utoaji hati kwa tija, wataongezewa vifaa na kuunda timu za kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao ikiwemo mtaa wa Mbondole kata ya Kivule.

Aidha, amewaasa watumishi wa sekta ya ardhi wanaotoa huduma kwa wananchi maeneo mbalimbali nchini, wasiwavuruge wananchi watoe huduma kadiri mwananchi anavyofika kwenye eneo la huduma ili kuondoa kero na kuweka utaratibu unaofaa kuwahudumia wananchi kulingana na walivyofika na kupata huduma kama serikali inavyoelekeza.

Kwa upande wake Bw. Juma Saidi Msimbazi mkazi wa Kivule ameridhishwa na huduma inayotolewa na Wizara ya Ardhi katika eneo lao kwa kuwasogezea huduma karibu zaidi na hali ikiendelea hivyo nchi itapiga hatua kubwa katika maendeleo.

Kliniki ya Ardhi kama hiyo ya Ilala Dar es Salaam inaendeshwa pia katika mikoa ya Dodoma, Mpunguzi, Mbeya, wilaya ya Mbarali na Shinyanga katika Manispaa ya Shinyanga na Wilaya ya Kahama.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga (katikati) akizungumza na wananchi Agosti 16, 2025 kwenye Kliniki ya Ardhi inayofanyika Kata ya Kivule Ilala Dar e salaam. Kulia ni Kamishna wa Ardhi Bw. Nathaniel Nhonge na kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Rehema Mwinuka.

Mwananchi akipata huduma kwenye Kliniki ya Ardhi inayofanyika Agosti 16, 2025 katika Kata ya Kivule Ilala Dar e salaam wa Kata ya Kivule Ilala Dar e salaam.

Baadhi ya wananchi wakiendelea kupata huduma kwenye Kliniki ya Ardhi inayofanyika Agosti 16, 2025 katika Kata ya Kivule Ilala Dar e salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga (wa pili kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Naibu Kamishna wa Ardhi Bw. Hussein Sadiki Iddi mara baada ya kuwasili eneo inapofanyika Kliniki ya Ardhi katika Kata ya Kivule Ilala Dar e salaam.

About the author

Alex Sonna