Featured Kitaifa

JKT,REA WAANZISHA UBIA WA KIHISTORIA:MRADI WA BILIONI TANO WA NISHATI SAFI KAMBI ZA  JKT

Written by Alex Sonna

Na Alex Sona, Dodoma

KATIKA  hatua inayoweza kuelezwa kama mpango wa kihistoria unaotarajiwa kubadilisha kabisa mfumo wa mapishi katika kambi za kijeshi, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeingia ubia na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kutekeleza mradi wa nishati safi wa Shilingi bilioni 5 wenye lengo la kuondoa matumizi ya kuni na mkaa hatua inayoleta usalama wa nishati, uhifadhi wa mazingira na ukuaji wa uchumi wa kijamii.

Hayo yameelezwa leo, Agosti 11, 2025, na Kanali Juma Mrai, Kaimu Mkuu wa Utawala wa JKT, wakati wa semina ya siku tatu iliyolenga kuwajengea uwezo watumishi 66 wa JKT kutoka kambi mbalimbali nchini, ili wawe na ujuzi unaohitajika kwa utekelezaji bora wa mradi wa nishati safi.

Amesema kuwa JKT imefikia asilimia 90 ya maandalizi ya kutekeleza mpango huo wa nishati safi ya kupikia na kwamba jeshi hilo limepanga kufikia malengo yake kabla ya muda wa mwisho wa mwaka 2034.

Kanali Mrai amebainisha kuwa awamu ya kwanza ya mradi ilianza Aprili 2025, ambapo REA tayari imetoa asilimia 50 ya fedha ilizoahidi na kwamba mradi umegawanywa katika awamu tatu, ambapo REA itatoa asilimia 30 katika awamu ya pili na asilimia 20 katika awamu ya tatu.

“Mnamo tarehe 4 Septemba mwaka huu, JKT ilisaini mkataba muhimu na REA, hatua iliyozindua mradi wa miaka miwili wenye lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kambi 22 za kijeshi ifikapo mwaka 2034,” amesema.

Ameeleza kuwa juhudi hizo za mageuzi zinafadhiliwa kwa kiwango kikubwa na REA, shirika la umma ambalo litatua asilimia 76 ya gharama zote za mradi, huku JKT ikichangia asilimia 24 zilizobaki.

“Ikumbukwe kuwa hatua hii inatokana na dhamira ya Serikali katika kukuza matumizi ya nishati safi, ambapo viongozi mbalimbali wamewahi kuweka mkazo kwa kueleza matumaini kwamba ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania watakuwa wamehamia kwenye nishati safi ya kupikia, “ameeleza na kuongeza kuwa;

Hili ni lengo lililowekwa kwenye Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), unaoungwa mkono na uwekezaji wa kimkakati kutoka REA na washirika wake, ” amesema.

Sambamba na mpango huu wa nishati safi,Kanali Mrai amesema REA pia imesaini makubaliano na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ili kuendeleza uzalishaji wa mkaa mbadala unaoitwa Rafiki Briquettes.

Mashine za kuzalisha mkaa huu rafiki wa mazingira tayari zimesambazwa katika kambi zote za JKT nchini.

Ushirikiano huu hauhusishi REA na JKT pekee, bali pia wadau muhimu kama vile Kampuni ya Kutengeneza Zana za Kishoka ya Tanzania (Kishoka Tools Manufacturers Group Company), Kampuni ya Envotec Services, na STAMICO, ambao wote wanachangia utekelezaji wa mradi huu muhimu.

Mhandisi Advera Mwijage, Mkurugenzi wa Teknolojia wa REA, amesisitiza dhamira ya wakala huo kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kusukuma ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Amesema Kupitia mpango huu, serikali imeelekeza taasisi zote zenye wafanyakazi zaidi ya 100 kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua inayoonyesha dhamira ya kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira.

About the author

Alex Sonna