Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele akimkakabidhi mkoba wenye fomu za kuomba kuteuliwa kuwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira. Mgombea huyo waaliambatana na Mgombea Mwenza, Amana Suleiman Mzee (kushoto) alichukua fomu hizo leo Agosti 11, 2025 ambapo Tume inataraji kufanya uteuzi Agosti 27 mwaka huu.
Na.Gideon Gregory-DODOMA
MGOMBEA urais kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira, amesema kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuongoza taifa, serikali yake itaweka kipaumbele katika kuimarisha ulinzi na usalama, kutoa elimu bure, na kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Rwamugira ametoa kauli hiyo leo Agosti 11,2025 mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma,aliyeambatana na mgombea mwenza wake, Amana Suleiman Mzee.
“Kuna vijana wengi waliomaliza vyuo vikuu na vya kati, lakini wako mtaani bila ajira. Sisi TLP tunakwenda kuimaliza changamoto hiyo,” amesema Rwamugira.
Aidha amesema kuwa TLP imelenga kuimarisha uchumi wa taifa ili kutoa nafasi nyingi zaidi za ajira kwa vijana, pamoja na kuweka mazingira rafiki ya kujiajiri kupitia ujuzi na maarifa ya kiufundi.
Akizungumzia sekta ya elimu, Rwamugira amesema kuwa serikali yake itajikita katika elimu ya ufundi stadi kuanzia ngazi za awali ili kuwapa wanafunzi ujuzi wa kujitegemea baada ya masomo yao, hatua ambayo pia inalenga kupunguza utegemezi wa ajira za ofisini.
Kuhusu sekta ya afya, amesema kuwa serikali ya TLP itaanzisha mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kwa wakati na kwa gharama nafuu.