Featured Kitaifa

WMA YAWAHAKIKISHIA WAKULIMA USAHIHI WA VIPIMO KATIKA UNUNUZI WA PAMBA

Written by Alex Sonna
KAIMU Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA Mkoa wa Simiyu, Bi. Happy Titi, akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la WMA kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma
Na.Alex Sonna-DODOMA

WAKALA wa Vipimo (WMA) umewatoa hofu wakulima wa zao la pamba kuhusu usahihi wa vipimo vinavyotumika katika ununuzi wa zao hilo, ukisisitiza kuwa vipimo hivyo vimehakikiwa na vinafuatiliwa kwa karibu ili kuzuia udanganyifu na kuwalinda walaji pamoja na wazalishaji.

Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 6,2025 na Kaimu Meneja wa WMA Mkoa wa Simiyu, Bi. Happy Titi, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la WMA kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
“Lengo kubwa la Wakala wa Vipimo ni kumlinda mlaji katika sekta ya afya, biashara, nishati na nyinginezo,” amesema Bi. Titi.

Ameeleza kuwa, kupitia ushiriki wao katika Maonesho ya Nanenane, WMA inatoa elimu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wadau wengine wa sekta mbalimbali kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo sahihi katika shughuli zao, ili kuhakikisha uadilifu na haki kwa pande zote.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Bi. Titi amesema kuwa elimu hiyo hutolewa kuanzia hatua za awali za maandalizi ya mashamba, ambapo maafisa wa WMA hushirikiana na wataalamu wa kilimo kuhakikisha vipimo vinavyotumika vimehakikiwa na kufuata viwango vya kitaifa na kimataifa.

“Kipimo chochote kabla hakijaanza kutumika ni lazima kipimwe. Wakaguzi wetu wanaendelea na ufuatiliaji kuhakikisha hakuna anayevunja sheria kwa kuchakachua vipimo,” amesisitiza.

Aidha, ametahadharisha kuwa wale wote watakaobainika kutumia vipimo visivyo halali watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kulipishwa faini au kufikishwa mahakamani.

Bi. Titi amesisitiza kuwa WMA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa vipimo katika sekta zote vinazingatia viwango sahihi kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.









About the author

Alex Sonna