Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama Cha Mapinduzi (UWT), Bi. Mary Chatanda, akizungumza na waandishi leo Agosti 1,2025 jijini Dodoma kuelekea Mkutano Maalum wa Kitaifa wa UWT unaotarajiwa kufanyika kesho Agosti 2,2025 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Dodoma.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama Cha Mapinduzi (UWT), Bi. Mary Chatanda, akizungumza na waandishi leo Agosti 1,2025 jijini Dodoma kuelekea Mkutano Maalum wa Kitaifa wa UWT unaotarajiwa kufanyika kesho Agosti 2,2025 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama Cha Mapinduzi (UWT), Bi. Mary Chatanda, ametoa onyo kali kwa wanachama watakaoshiriki katika Mkutano Maalum wa Kitaifa wa UWT unaotarajiwa kufanyika kesho, kuacha mara moja kujihusisha na vitendo vya rushwa, katika kipindi hiki cha kuelekea kura za maoni za kuwapata wagombea wa Viti Maalum kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 1, 2025 jijini Dodoma, Bi. Chatanda amewasihi wajumbe wapiga kura kufanya maamuzi yao kwa kuzingatia sifa na uwezo wa wagombea badala ya kushawishiwa kwa fedha au vishawishi vya aina yoyote.
“Chama kimeweka wazi msimamo wake. Tunapambana na ufisadi katika ngazi zote. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kupiga vita rushwa wakati wa chaguzi. Kama UWT, tunatoa wito huo huo—chagueni wagombea kwa haki, si kwa sababu ya kutoa fedha,” amesema Bi. Chatanda.
Zoezi la kupiga kura linatarajiwa kufanyika kesho, Agosti 2, 2025, katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC), na litahusisha makundi manne maalum: Asasi za Kiraia (NGOs), wafanyakazi, wasomi wa vyuo vikuu, na watu wenye ulemavu. Jumla ya wagombea 32 wanatarajiwa kushiriki, ambapo wanane kutoka kila kundi watateuliwa.
Bi. Chatanda ameainisha kuwa kundi la watu wenye ulemavu linajumuisha wagombea watatu kutoka Tanzania Bara na mmoja kutoka Zanzibar. Kundi la wafanyakazi lina wagombea wawili kutoka Bara na mmoja kutoka Zanzibar; wasomi wa vyuo vikuu watatu kutoka Bara na mmoja kutoka Zanzibar; huku kundi la NGOs likiwa na wawili kutoka Bara na mmoja kutoka Zanzibar.
Zaidi ya wanachama 1,200 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanatarajiwa kushiriki katika mchakato huo muhimu wa kura za maoni.
Ameongeza kuwa uteuzi rasmi wa wagombea wa Viti Maalum utafanyika tu baada ya chama kushinda katika uchaguzi mkuu ujao, iwe ni nafasi za ubunge, udiwani au urais.
“Mgombea ambaye hatashiriki kikamilifu katika kampeni za chama wala kuchangia ushindi wa CCM kwenye ngazi mbalimbali, asitarajie kuteuliwa. Hii ni muhimu hasa endapo idadi ya viti itakuwa ndogo,” amesisitiza.