Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makala, akziungumza na Waandishi wa habari leo Julai 18,2025 Jijini Dodoma kuhusu maandalizi ya mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge,uwakilishi na Udiwani.
Na.Alex Sonna_DODOMA
KIKAO cha mwisho cha uteuzi watia nia walioomba kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa kitafanyika Julai 28 mwaka huu.
Kikao hicho kitatanguliwa na Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kisha kufuatiwa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM vitakavyofanyika Julai 26 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 19,2025 Jijini Dodoma, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amos Makala, amesa kuwa maandalizi ya mchakato wa uteuzi yanaendelea vizuri.
“Wagombea ni wengi, kazi kubwa imefanyika kwani tunataka haki itendeke kwa kufanya uteuzi makini, hivyo tumejipa nafasi mpaka tarehe 28.
Amesisitiza : “CCM ni Chama makini chenye uzoefu na baada ya uteuzi kukamilika ratiba kuhusu kura za maoni itatolewa.”
Aidha CPA Makalla,amesema kuwa mpaka sasa hakuna mgombea aliyekatwa katika mchakato wa uteuzi kama ambavyo baadhi ya watu wanavyodai.
“Taratibu za Chama zinaeleweka kwani vikao vya mwisho vya uteuzi bado havijafanyika. Ndiyo maana wakati wa kuchukua fomu tukakataza watia nia wasije na matarumbeta maana watu wataanza kuhoji nani aliyekuja na matarumbeta au wapambe wengi.
CPA Makala aliongeza kuwa: “Wanachama na wagombea watulie, hakuna mtu aliyekatwa au kufyekwa. Tarehe 28 ndipo kutafanyika kikao cha mwisho cha uteuzi wa wagombea.”
Awali, vikao hivyo vilipangwa kufanyika jana na leo ambapo majina matatu yalitarajiwa kupitishwa katika kila nafasi kisha wanachama kuyapigia kura za maoni.
Tangu kuanza mchakato wa kuwapata wagombea ngazi mbalimbali kwa ajili ya kukiwakilisha CCM katika uchaguzi mkuu, idadi kubwa ya wanachama wamejitokeza.
Wanachama na makada wa CCM walioonesha nia kugombea nafasi hizo ilikuwa zaidi ya 30,000 katika kata 3,660 na majimbo 272.