MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 18,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hasan kwa kipindi cha miaka minne.


MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 18,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hasan kwa kipindi cha miaka minne.
Na Alex Sonna-DODOMA
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Mara umetekeleza miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya kila mwananchi kwa kugusa sekta muhimu za kijamii ikiwemo maji, elimu, na afya.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi amesema Mkoa umetekeleza miradi 91 ya maji, ambapo miradi 58 imekamilika na 33 inaendelea kutekelezwa. Aidha, kupitia mpango wa BOOST na SEQUIP, madarasa 1,259 ya msingi na madarasa 310 ya sekondari yamejengwa, sambamba na ujenzi wa shule mpya 15 za sekondari na shule 2 za amali.
Akizungumza leo Julai 18,2025 Jijini Dodoma na waandishi wa habari amesema Katika sekta ya afya, Mkoa umefanikiwa kuboresha huduma kwa kujenga hospitali mpya 7 za wilaya, vituo vya afya 12, na kukarabati zaidi ya zahanati 40, hatua ambayo imepunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi waishio vijijini.
“Kabla ya mwaka 2021, baadhi ya wilaya kama Serengeti, Bunda na Tarime zilikuwa na changamoto kubwa ya vituo vya afya. Kupitia mpango wa serikali wa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati na kila kata inakuwa na kituo cha afya, huduma sasa zimesogezwa karibu na wananchi, “amesema na kuongeza;.
“Tumeweza kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma kutoka 227 hadi 281 ndani ya miaka minne. Hii ni hatua kubwa sana kwa Mkoa wetu,” amesema Kanali Mtambi.
Amesema Mpango wa Serikali wa kuongeza uandikishaji na kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani umeleta mafanikio makubwa ambapo Madarasa yaliyojengwa kupitia BOOST na SEQUIP yamepunguza wastani wa wanafunzi kwa darasa kutoka 90 hadi 45 katika baadhi ya shule.
Pia, shule za sekondari za wasichana zimeongeza uandikishaji wa watoto wa kike kutoka maeneo ya mbali, na kuwaweka katika mazingira salama ya kujifunza.
“Wanawake na watoto wamekuwa wakihangaika kwa muda mrefu kusaka maji, hali ambayo ilileta madhara ya kiafya na kupunguza muda wa kushiriki shughuli za kiuchumi,hivi sasa, kupitia miradi 91 ya maji, vijiji zaidi ya 100 vimeunganishwa na huduma ya maji ya bomba au visima virefu.