Na Gideon Gregory, Dodoma
Katika jamii nyingi, ukatili mara nyingi huzingatiwa kama kitendo cha mwili kinachoonyesha kuumiza mtu kwa njia za moja kwa moja kama vile kumpiga, kumchapa, au kumjeruhi.
Hata hivyo, ukatili wa kihisia ni aina ya ukatili ambao mara nyingi haionwi au kueleweka kwa urahisi, lakini athari zake kwa wahusika ni za kina na zinaweza kuathiri maisha yao kwa muda mrefu.
Ukatili wa kihisia ni silaha iliyosahaulika katika ndoa au mahusiano ambapo imesababisha maumivu yasiyoonekana lakini yenye nguvu kubwa.
Ukatili wa kihisia unahusisha matendo au maneno yanayolenga kudhoofisha hali ya kihisia, utu, au heshima ya mtu katika mahusiano ya karibu, hasa ndoa au uhusiano wa mapenzi ambao unaweza kuwa kama kusemwa maneno mabaya au kuonesha upendeleo wa kuumiza kihisia, kudharau, kuwatukana, au kupuuza hisia za mwenza wako.
Katika safari yangu ya kutafuta kuelewa sababu ya hali hii, Jambo FM imezungumza na baadhi ya wanandoa ambao.
Kila mmoja alikuwa na sababu zake Wengine walikiri kuwa hayo ni maneno ya kawaida au sehemu ya maisha ya ndoa, lakini waliishia kugundua kuwa mioyo yao imevunjwa vunjwa vipande vilivyojaa maumivu huku wakielezea visababishi vya tatizo hilo.
Mwanandoa wa kwanza (mwanamke) ambaye hakutaka kutaja jina lake anasema hali hiyo hitokea pale ambapo mmoja wao anakuwa amepata mtu mwingine hali inayosababisha mambo hayo kuanza kutokea kwenye ndoa au mahusiano japo inategemea anaweza kuwa mwanaume au mwanamke.
“Unakuta mwanaume na mwanamke kila mmoja ana mtu wake pembeni, kwahiyo sasa wa ndani anamuona sasa hana thamani, kwahiyo mara nyingi inakuwaga hivyo mara nyingi inakuwaga hivyo ndiyo maana wanatoleana maneno kama hayo,”amesema.
Mwanandoa wa Pili (mwanaume) yeye anadai kuwa kwanza kampani anazokuwa nazo mwanamke (mashoga zake), vijistori wanavyokuwa wanapiga ndipo anachukua tabia hizo ambazo hupelekea unyanyasaji huo kuanza kwenye ndoa au mahusiano.
“Anategeshea mwanaume wake akifanya kosa kidogo analianzisha yaani anapita mule mule ambapo walikuwa wanazungumza na mashoga zake ambavyo walikuwa wanamshauri, si unajua wanaigana wanawake kwahiyo mojawapo ya sababu ndo hiyo,”amesema.
Mwanandoa huyo anaendelea kusema kuwa hata suala la uchumi nalo ni chanzo kwasababu hakuna mwanamke anapenda kuona mwanaume ambaye hajiwezi fedha (hoi hae).
Mwanandoa wa kwanza anaendelea kusema kuwa mwenza unakuta alikuwa na upendo lakini akapunguza, sasa katika kufanya hivyo anajikuta analeta kelele ambazo mmoja wao anazivumilia mpaka anazichoka.
“Kwahiyo nikishazichoka basi nitakuwa naona mbona huyu kama ananionea,”anasema mwanandoa wa kwanza.
Mwanandoa wa Pili anaongeza kuwa kila mtu kaumbwa na nidhamu yake hivyo hadhani kama kushuka kiuchumi inaweza kuwa sababu ya kurushiana maneno.
Lugha za fedheha zinazotweza utu wa binadamu zimekua kama silaha inayotumka kupima uzito, hadhi ya mtu hata thamani yake, na pengine wengi wetu hatujui kwamba mara nyingi, mtu anayevumilia lugha hizo za kejeli katika mahusiano basi tayari amechoka na siyo kwamba amezoea la hasha.
Niliamua kumtafuta mtaalamu wa saikolojia na unasihi Peter Njau, nikihitaji kujua ni athari gani anaweza kuzipata mtu anayepitia ukatili wa kihisia yaani lugha zisizo na staha zenye kuuthi na kutweza utu?
Bw. Njau anasema athari za kutumia lugha ambazo hazina staha miongoni mwa wanandoa au wana jamii ambazo zinatweza utu moja kwa moja zinaweza kuwa ana athari nyingi ikiwemo zile zinazooneka na zisizoonekana ikiwa ni pamoja na kupunguza kujiamini.
“Mfano unakuta mtu amekosolewa labda kupitia maumbile yake, rangi yake, muonekano wake jinsi alivyo hata kiwango chake cha kujiamini kinaweza kikashuka, kwamba ameambiwa maneno ambayo sio mazuri na mwenza wake na huu unakuwa ni ukatili,”anasema Bw. Njau.
Anasema huo unakuwa ni ukatili wa maneno, kwamba mtu anakuwa hajaguswa kimwili lakini umempa maneno ambayo yameenda kuathiri hisia zake,”anasema.
Kwa sababu madhara ya ukatili huu siyo ya kawaida inanibidi kumtafuta kiongozi wa dini kwa lengo la kupata somo juu ya namna wanandoa wanapaswa kuwa na mazungumzo yenye staha yaani mbinu bora za mawasiliani (marriage communication).
Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kiwanja cha Ndege Padre Pascal Dionese anawashauri wanandoa au wapenzi pale wanapozungumza kujaribu kuepuka maneno yele yenye matusi au kupigiana kelele pasipokuwa na sababu pamoja na kwamba watakuwa na hasira kwasababu vikombe viwili vinapokuwa kwenye sinia moja havikosi kugongana.
“Lakini ninyi kama ninyi mjitahidi kuepuka mazingira kama hayo, pia katika mazungumzo yenu muwe na dhana ya kusikilizana, kwasababu huwezi ukawa na mawasiliano chanya kama hakuna kusikilizana, basi kumbe kuna baadhi ya vitu lazima mviepuke katika ndoa au mahusiano yenu,”amesema.
Ukatili wa kihisia ni tatizo linalozidi kuenea na kuathiri maisha ya watu wengi katika ndoa na mahusiano ya karibu, ni silaha iliyosahaulika ambayo inaweza kuua hisia na kuangamiza maisha ya furaha na amani.
Hivyo basi, ni muhimu kwa jamii kuelimika, watu kuweza kutambua dalili za ukatili huu na kutoa msaada wa haraka ili kuokoa maisha na mahusiano yenye afya.