Featured Kitaifa

WANANCHI WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UCHIMBAJI WA MADINI YA BATI MKOANI KAGERA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Wananchi wametakiwa kuchangamkia fursa za uwekezaji katika uchimbaji wa madini ya bati yanayopatikana kwa wingi katika Mkoa wa Kagera, hususan katika Wilaya ya Kyerwa, kufuatia mahitaji makubwa ya madini hayo ndani na nje ya nchi.

Wito huo umetolewa leo na Mkaguzi Msaidizi wa Madini kutoka Ofisi ya Afisa Mgodi Mkazi – Kyerwa, Gilbert Fumbo, alipokuwa akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Fumbo amesema kuwa Mkoa wa Kagera umejaliwa kuwa na madini mengi ya bati yanayopatikana katika maeneo ya Kyerwa, Sindicate, Kabingo, Murongo, Katera na Kaitambuzi, akibainisha kuwa bado kuna fursa kubwa kwa wananchi na wawekezaji kuchukua hatua za uwekezaji.

“Mahitaji ya madini ya bati katika soko la kimataifa ni makubwa ikilinganishwa na idadi ya wachimbaji waliopo kwa sasa. Tunawahamasisha wananchi kujitokeza kuomba leseni za uchimbaji wa madini na kuanza shughuli rasmi za uchimbaji ili kujiongezea kipato, kuchangia mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa nchi,” ameeleza Fumbo.

Ameongeza kuwa azma ya Serikali kupitia kaulimbiu ya “Madini ni Maisha na Utajiri” inalenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini. Amebainisha kuwa Ofisi ya Madini Mkoa wa Kagera imejipanga kikamilifu kutangaza fursa za uwekezaji ili kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha Watanzania.

Fumbo pia ameeleza kuwa kutokana na jitihada za Tume ya Madini za kuhamasisha uwekezaji, wawekezaji kutoka mataifa ya China, Korea na Urusi wameanza kujitokeza kwa wingi katika shughuli za uchimbaji wa madini ya bati tangu mwaka 2024.

Kuhusu mchango wa madini hayo kwenye makusanyo ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Fumbo amebainisha kuwa madini ya bati yamechangia shilingi bilioni 1.423, sawa na asilimia 94.86 ya lengo la ukusanyaji wa shilingi bilioni 1.5 la madini hayo.

Katika hatua nyingine, Fumbo ameainisha uwepo wa madini mengine muhimu kama tungsten yanayopatikana katika eneo la Kigorogoro, ambayo hutumika kutengeneza vifaa vya kivita na kielektroniki, na kuwahamasisha wananchi kuchangamkia pia fursa za uchimbaji wa madini hayo.

“Kagera siyo tu ina utajiri wa ardhi yenye rutuba, bali pia ina hazina kubwa ya madini ambayo tukiyatumia vyema, yanaweza kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa jamii na taifa kwa ujumla,” amehitimisha Fumbo.

About the author

mzalendo