Featured Kitaifa

RC KATAVI ABAINISHA MAFANIKIO MAKUBWA YALIYOFANYWA NA  SERIKALI YA AWAMU SITA

Written by mzalendoeditor

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hoza Mrindoko,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 3,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .

 

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hoza Mrindoko,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 3,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hoza Mrindoko,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 3,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .

Na.Alex Sonna-Dodoma

 

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Hoza Mrindoko amesema kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia biashara ya kaboni (hewa ukaa) yameleta mapinduzi ya maendeleo katika Mkoa huo hususan Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

Mhe. Mrindoko,ameyasema hayo leo Julai 3,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .

Mhe.Mrindoko amesema hadi kufikia Juni 2025, mkoa umepata mapato ya jumla ya Shilingi 25,293,421,607.17 kutoka biashara hiyo ya kimazingira, fedha ambazo zimeelekezwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

“Kupitia fedha hizo, Mkoa umeweza kujenga madarasa 52 na kukarabati madarasa 20, kujenga nyumba 5 za walimu kwa mfumo wa 2 kwa 1 na nyumba moja ya walimu kwa mfumo wa 3 kwa 1.”amesema Mrindoko

Aidha amesema vichomea taka sita (incinerators) vimejengwa kwenye vituo vya afya, pamoja na mashimo sita ya kondo la mama (placenta pits) kwa ajili ya huduma bora za uzazi ikiwa ni pamoja na matundu 128 ya vyoo kujengwa, madawati 1,496 yametengenezwa, na ofisi nane za vijiji pamoja na masoko mawili ya vijiji yamekamilika.

“Biashara hiyo pia imezalisha ajira 112 kwa vijana wanaolinda misitu, kaya 4,400 zimepatiwa kadi za bima ya afya (CHF iliyoboreshwa), walimu 20 wa mkataba wameajiriwa na shule 16 zimepatiwa chakula kwa ajili ya wanafunzi.”amesema 

Amesema Wanawake wajasiriamali pia wamenufaika kupitia mikopo ya jumla ya Shilingi 117,213,800.00.

Aidha, fedha nyingine kiasi cha Shilingi bilioni 2.78 zilizopokelewa Aprili 2025, zimepangwa kutumika kuendeleza miundombinu ya elimu, kutoa ajira kwa walimu na wahudumu wa afya, pamoja na kuimarisha uhifadhi wa misitu.

Pia ameeleza kuwa katika sekta ya kilimo, ukarabati wa skimu za umwagiliaji za Mwamkulu na Kabage unaoendelea umegharimu Shilingi bilioni 54.68 na utekelezaji wake umefikia asilimia 22.5 ambapo kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 2,700 hadi 6,000 na kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka gunia 10 hadi 60 kwa ekari.

Amesema Eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka hekari 36,687 mwaka 2021 hadi hekari 267,680 mwaka 2025, huku vijana 756 wakipewa mafunzo ya ujenzi wa vitalu nyumba na Idadi ya vyama vya ushirika imeongezeka kutoka 36 vya mwaka 2021 hadi 56 mwaka 2025, huku wanachama wakiongezeka kutoka 18,340 hadi 25,320.

Kwa upande wa miundombinu ya kimkakati, Mkuu huyo wa mkoa wa katavi amesema Mkoa umefanikiwa kukamilisha ujenzi wa barabara muhimu zikiwemo Mpanda–Tabora (km 337), Mpanda–Vikonge (km 39.5), na Mpanda–Sitalike (km 37) na Ku ongeza kuwa Ujenzi unaendelea katika barabara ya Vikonge–Luhafwe (km 25), Kibaoni–Sitalike (km 50), na Luhafwe–Mishamo (km 37.35).

Katika sekta ya madaraja, amesema Daraja la Kavuu lenye urefu wa mita 84 linaendelea kujengwa, huku Daraja la Msadya (mita 60) likiwa limekamilika na linatumika.

Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa, kupitia mikakati ya Serikali, Shule ya Kanda ya Wavulana imepokea Shilingi bilioni 4.1, huku Shule Maalum ya Wasichana iliyopo Halmashauri ya Nsimbo ikipokea zaidi ya Shilingi bilioni 4. Katika hatua ya kuboresha elimu, shule mpya 129 zimejengwa (sekondari 32 na msingi 97) kupitia programu mbalimbali kama BOOST, UVIKO, SEQUIP, GPE, LANES, P4R, pamoja na fedha za Serikali Kuu na Halmashauri. Katika sekta ya maji, Mradi wa Maji wa Miji 28 katika Manispaa ya Mpanda unaendelea kutekelezwa.

Sekta ya afya nayo imepata mafanikio ambapo ameeleza kuwa jumla ya miradi 22 mipya inatekelezwa ikiwemo Hospitali ya Rufaa 1, Hospitali 4 za Halmashauri, Vituo vya Afya 10 na Zahanati 7. Kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA III), vijiji 58 vimeunganishwa na huduma ya umeme, na kwa sasa vijiji vyote 172 vya Mkoa wa Katavi vina umeme.

Aidha Vitongoji 504 kati ya 912 tayari vimepata huduma hiyo, na vitongoji 408 vilivyobaki vitafikiwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Ameitaja Miradi mingine mikubwa iliyotekelezwa ni pamoja na kukamilika kwa Bandari ya Karema, utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji ya Mwamkulu na Kabage, zaidi ya miradi 200 inayogharamiwa na fedha za kaboni, ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya za Tanganyika na Mlele, ujenzi wa ghala, vihenge na ofisi za NFRA, pamoja na ukarabati wa reli ya Kaliuwa–Mpanda (km 210).

About the author

mzalendoeditor