Featured Kitaifa

WATUMISHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS WAHIMIZWA USHIRIKIANO NA WIZARA ZA KISEKTA

Written by mzalendoeditor

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja akifungua kikao kazi cha kimkakati na Menejimenti na watumishi wa Ofisi hiyo leo Jumatano (Julai 2, 2025) jijini Dodoma kilicholenga kujadili vipaumbele vya mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi hiyo katika mwaka 2025/2026.

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamuwa Rais, Prof. Peter Msoffe akizungumza wakati wa kikao kazi cha kimkakati na Menejimenti na watumishi wa Ofisi hiyo leo Jumatano (Julai 2, 2025) jijini Dodoma kilicholenga kujadili vipaumbele vya mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi hiyo katika mwaka 2025/2026.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakim Zahabu akiwa katika kikao kazi cha kimkakati na Menejimenti na watumishi wa Ofisi hiyo leo Jumatano (Julai 2, 2025) jijini Dodoma kilicholenga kujadili vipaumbele vya mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi hiyo katika mwaka 2025/2026. 

Sehemu ya Watendaji wa Ofiisi ya Makamu wa Rais wakifuatilia kikao kazi cha kimkakati kilichofanyika leo Jumatano (Julai 2, 2025) jijini Dodoma kilicholenga kujadili vipaumbele vya mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi hiyo katika mwaka 2025/2026.

……

WATUMISHI wa Ofisi ya Makamu wa Rais wamehimizwa kuimarisha ushirikiano na mahusiano na Wizara, Taasisi na Idara za kisekta ili kuwezesha kuimarika kwa Muungano na usimamizi endelevu wa sekta ya hifadhi ya mazingira nchini.

Rai hiyo imetolewa leo Jumatano (Julai 2, 2025) jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Mhandisi Cyprian Luhemeja wakati akifungua kikao kazi cha kimkakati kinacholenga kujadili vipaumbele vya mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Ofisi hiyo katika mwaka wa fedha 2025/26.

Mhandisi Luhemeja amesema kikao hicho ni mkakati maalum wa Ofisi hiyo katika kujiwekea malengo mahsusi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na hivyo kuwashirikisha watumishi wa kutambua wajibu na majukumu waliyonayo ili kufikia malengo.

Amebainisha kuwa katika mwaka wa Fedha 2025/2026 vipaumbele vya ofisi hiyo ni kuhakikisha inapatia majibu hoja mbalimbali kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira kupitia ushirikiano na wadau wa kimkakati ikiwemo Wizara, Taasisi na Idara za kisekta.

“Ni wajibu wetu kuhakikisha tunaimarisha uratibu na ushirikiano na Wizara, Idara na Taasisi zote za kisekta ili kuhakikisha tunatambulika vyema….kwa mfano masuala ya uchumi wa buluu kunahitajika usimamizi na uratibu wetu wa karibu ili kuweza kutekeleza kwa pamoja na wizara nyingine,” amesema Mhandisi Luhemeja.

Mhandisi Luhemaja amesema mazingira ni sekta mtambuka inayogusa wadau wote wa kimkakati zikiwemo Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika na Taasisi za umma, hivyo ofisi hiyo ina wajibu wa kusimamia uratibu wa miongozo mahsusi ya masuala ya uhifadhi wa mazingira nchini.

Amesema kuwa ili kufikia malengo ya uratibu wa masuala ya mazingira nchini, ofisi hiyo imechukua hatua mahsusi ikiwemo kuunda madawati maalum ya uratibu wa masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira katika mashirika na taasisi za umma pamoja na mamlaka za serikali za mitaa nchini.

“Kuna zaidi ya mashirika na taasisi za umma 302 ambazo zina idara ya mazingira…tumeanza kushirikiana katika kuhimiza masuala ya uhifadhi wa mazingira kwa kutumia fursa zilizopo…ushirikiano huu na wadau ni muhimu katika kuchagiza agenda ya mazingira nchini” amesema Luhemeja.

Kuhusu maudhui ya mpango kazi uliondaliwa kwa mwaka 2025/26, Mhandisi Luhemeja, amesema vipaumbele na mwelekeo wake umejikita katika kuleta matokeo tarajiwa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya ofisi hiyo katika kufikia malengo yaliyowekwa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe amesema watendaji na watumishi wa ofisi hiyo wapo tayari katika kutekeleza maelekezo yaliyotolewa kupitia kikao hicho ili kubadilisha mfumo wa utendaji kazi wenye kuleta matokeo chanya kwa umma.

Kikao hicho cha siku 03 kitahusisha mawasilisho ya mada mbalimbali za masuala ya Muungano na Mazingira sambamba na kujadili Mpango wa tathimini na ufuatiliaji wa shughuli na majukumu ya ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26.

About the author

mzalendoeditor