Featured Kitaifa

HUDUMA ZA AFYA ZABORESHA MAISHA KAGERA,SHULE NA UMEME VYAPELEKEA MAGEUZI YA HARAKA

Written by mzalendoeditor

MKUU  wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 1,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .

Na Alex Sonna-DODOMA
MAGEUZI  makubwa ya sekta ya afya yamechochea mabadiliko ya maisha kwa maelfu ya wananchi wa Kagera baada ya hospitali, vituo vya afya na zahanati kusogezwa karibu na wananchi kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo awali.
Hayo yamesemwa na  Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa,wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 1,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .
Mhe.Mwassa  amesema kati ya mwaka 2020 hadi Aprili 2025, Mkoa umefanikiwa kuongeza hospitali kutoka tatu hadi 11, vituo vya afya kutoka 29 hadi 42 na zahanati kutoka 217 hadi 283, hatua ambayo imepunguza umbali wa wananchi kufuata huduma na kuokoa maisha kwa wakati.
Amesema huduma za kibingwa kama upasuaji wa masikio, koo na pua (ENT), magonjwa ya ndani na mifupa sasa zinapatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, jambo lililosababisha ongezeko kubwa la wagonjwa wanaopata huduma ndani ya mkoa na kupunguza utegemezi wa mikoa mingine.
“Matibabu yaliyokuwa yakisubiri rufaa kwenda Bugando au Muhimbili, leo hii yanapatikana Bukoba,Wagonjwa sasa wanapata tiba kwa wakati, karibu na familia zao,” amesema.
Katika sekta ya elimu, Mkuu huyo wa Mkoa amesema shule mpya za msingi, sekondari na vyuo vya VETA zimeongezeka kwa kasi, ikiwa ni pamoja na shule ya bweni ya wasichana ya Kagera River na chuo cha ufundi cha Burugo, ambacho ni cha kisasa na kimeongeza nafasi kwa vijana wa mkoa huo kupata elimu ya ufundi stadi.
Pia amesema mafanikio makubwa yamepatikana kwenye upatikanaji wa maji safi na salama, ambapo huduma hiyo imefikia zaidi ya asilimia 90 katika maeneo ya mijini na vijijini. Mradi wa Kyaka–Bunazi, pamoja na ule wa Kemondo, ni miongoni mwa miradi mikubwa iliyotekelezwa kwa mafanikio.
Kwa upande wa nishati, Mwassa amesema Mkoa wa Kagera sasa umeandika historia kwa kuwa na umeme katika vijiji vyote 662 kwa mara ya kwanza. Hali hiyo imeleta nuru kwa kaya, mashule, zahanati na miradi midogo ya uzalishaji.
Ameeleza kuwa barabara na madaraja mapya yamefungua miji na vijiji kwa urahisi wa usafiri na biashara, huku sekta ya kilimo cha kahawa ikinufaika na mageuzi ya bei na uzalishaji baada ya kuondolewa kwa tozo kandamizi.
Katika kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja, mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu imekuwa msaada mkubwa, na kaya maskini zaidi ya 380,000 zimelindwa kupitia mpango wa TASAF.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Kagera mesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu miradi yote na kuhakikisha kuwa maendeleo yanawagusa watu wa kada zote kwa usawa na haki.
“Tumejifunza kuwa huduma bora zinapowafikia wananchi, maisha hubadilika kwa haraka,huu ni mwanzo tu wa safari yetu ya maendeleo,” amesema.

About the author

mzalendoeditor