Featured Kitaifa

USALAMA WA WATOTO WAKATI WA SAFARI NI WETU SOTE.

Written by mzalendoeditor
Issa Mwadangala.

Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe wametoa elimu juu ya usalama wa watoto wakiwa safarini kwa watoa huduma ya usafirishaji wa abiria walipokuwepo eneo la kukagulia magari Chimbuya lililopo Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Akizungumza Juni 30, 2025 na abiria pamoja na madereva katika ukaguzi huo Mkaguzi wa Polisi Nelson Mwinuka alibaini watoto waliokuwa wakisafirishwa kwa msongamano mkubwa ndani ya gari dogo lenye usajili namba T.461  CGE aina ya hiace zaidi ya watoto 38 lilikuwa limepakia, hali ambayo ni hatari kwa maisha yao na aliwataka kuacha tabia hiyo mara moja ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

“Kuzidisha abiria ni kosa la kisheria na ni hatari kwa maisha ya watu, hususani watoto, msiwabebe watoto kama mizigo kwani wanahitaji usalama sawa na watu wazima. Kila dereva anatakiwa kuhakikisha abiria anakaa katika nafasi salama inayotakiwa kisheria.” alisema Mkaguzi Mwinuka.

“Wazazi na walezi mnapaswa kupaza sauti juu ya jambo hili ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikiaha mahakamani bila kusahau kuwaelimisha kutambua mazingira hatarishi na kuwa na ujasiri wa kusema ‘hapana’ panapokosekana usalama wa watoto pindi mnaposafiri nao” alisisitiza Mkaguzi Mwinuka.

Jeshi la Polisi linaendelea kuikumbusha jamii kuwa usalama wa watoto ni jukumu la kila mmoja na kuwaomba wananchi kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapoona viashiria vya usafirishaji hatarishi au ukiukwaji wa sheria barabarani.

Kwa upande wa abiria na madereva hao waliungana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kwa pamoja walisema ni jukumu lao watoto kuwa salama si tu nyumbani bali hata wakiwa wanasafiri kwa manufaa ya taifa la kesho.
WhatsApp Image 2025-06-30 at 11.14.51_6a32d24d.jpg
WhatsApp Image 2025-06-30 at 11.14.52_ff91e2cf.jpg
PICHANI NI MKAGUZI WA POLISI NELSON MWINUKA AKITOA ELIMU KWA WAZAZI, WALEZI IKIWA NI PAMOJA NA MADEREVA

About the author

mzalendoeditor