Featured Kitaifa

MMILIKI MWANAMKE AONGOZA MAGEUZI YA UCHIMBAJI WA SHABA MPWAPWA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Mpwapwa

Mmiliki wa mgodi wa Ikombo Hill uliopo katika Kijiji cha Matonya, Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Bi. Doreen Kissia, ameibuka kuwa mfano wa kuigwa katika sekta ya uchimbaji wa madini ya shaba, akiwa mwanamke pekee anayeongoza mgodi unaotoa ajira kwa zaidi ya asilimia 98 ya wakazi wa vijiji vya Matonya na Kinusi.

Bi. Doreen ameonesha uongozi bora na ubunifu kwa kufanikisha ujenzi wa barabara ya kilomita moja inayounganisha mgodi huo na barabara kuu, jambo lililorahisisha usafirishaji wa madini. Kwa sasa, mgodi huo unazalisha wastani wa tani 30 za madini ya shaba kwa mwezi.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Bi. Doreen ameiomba Serikali kusaidia kupeleka umeme katika mgodi wake ili kupunguza gharama kubwa za uendeshaji zinazotokana na matumizi ya jenereta.

Kwa upande wake, Mhandisi Chacha Megewa wa Tume ya Madini, ametoa elimu kwa Bi. Doreen na wachimbaji wengine kuhusu umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya uchenjuaji. Amebainisha kuwa changamoto kubwa kwa wachimbaji wa shaba ni ukosefu wa teknolojia hiyo, hali inayosababisha mawe yenye kiwango kidogo cha shaba (low grade) kutupwa.

“Teknolojia ya uchenjuaji haimaanishi lazima uwe na mtambo mkubwa. Hata kiwanda kidogo kinaweza kuongeza thamani ya madini. Ukiweka mtambo mgodini, unapunguza pia gharama za kusafirisha malighafi kwenda viwandani,” amesema Mhandisi Chacha.

Ameeleza kuwa kupitia teknolojia hiyo, inawezekana kuongeza kiwango cha shaba kutoka asilimia 1 hadi 20, na kuuza madini hayo kama ‘cathode’ badala ya kuyauza kama malighafi ghafi.

Naye Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini, Bw. Fahad Mkuu, amewahimiza wachimbaji kutowahusisha watoto katika shughuli za migodini kutokana na hatari zake kwa watoto. Pia amesisitiza umuhimu wa kuweka akiba na kutumia mapato yao kwa maendeleo ya familia na vijiji badala ya matumizi yasiyo ya lazima.

Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi ya Mkoa wa Dodoma, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), inaendelea kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini ya kimkakati kama shaba kupitia mradi wa kuendeleza madini yaliyosahaulika. Mradi huu umetajwa kuwa mkombozi kwa kuwapatia wachimbaji elimu, ushauri wa kitaalamu, na mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali katika Sekta ya Madini.

About the author

mzalendo