Featured Kitaifa

MAVUNDE ATIMIZA NDOTO ILIYOMUUMIZA KWA  MIAKA 15, AZINDUA JENGO LA KUPUMZIKIA HOSPITALI YA RUFAA DODOMA

Written by mzalendoeditor
Mbunge wa Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde,akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo  la kupumzikia  ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma hafla iliyofanyika leo Juni 25,2025 jijini Dodoma.
Na Alex Sonna, Dodoma
Kwa mara nyingine, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini ambaye pia ni Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ameandika historia kwa vitendo kwa kuzindua rasmi jengo la kisasa la kupumzikia ndugu wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma hatua inayoakisi dhamira yake ya dhati ya kuhudumia jamii.
Uzinduzi wa jengo hilo umefanyika Juni 25, 2025, mbele ya wananchi, viongozi na wadau mbalimbali wa afya, ambapo Mavunde alieleza kuwa ujenzi huo ni sehemu ya kutimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kuwasaidia wananchi kupata mahala salama na stahiki pa kupumzika wanapouguza wapendwa wao.
“Tangu mwaka 2010 nilipojitokeza kwa mara ya kwanza kuwania ubunge, nilitamani sana kupata fursa ya kuwa kiongozi katika eneo nilikozaliwa ili niweze kuchangia maendeleo ya watu wangu,” amesema Mavunde huku akifichua kuwa tukio la kushuhudia wagonjwa na ndugu zao wakilala nje ya geti la hospitali usiku ndilo lililomgusa zaidi na kumhamasisha kuanzisha mpango huo.
Jengo hilo lina mabenchi 24, televisheni kwa ajili ya taarifa muhimu na uzio kwa usalama. 
Aidha, amesema asilimia kubwa ya wanaopumzika hospitalini hapo si wakazi wa Dodoma bali ni wanaotoka mikoa mbalimbali, hali iliyomfanya kuchukua hatua hiyo kama mchango wa kibinadamu kwa taifa.
Mavunde amesema juhudi hizo ni sehemu ya mtazamo wake wa kuwa “mtumishi wa watu” na si kiongozi wa jina tu. 
Amekumbushia hatua mbalimbali alizochukua tangu mwaka 2015 ikiwa ni pamoja na kufunga kamera na maikrofoni katika maeneo ya kutolea huduma ili kuimarisha uwajibikaji kwa watumishi wa afya.
Katika hatua nyingine, ametoa rai kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuwaangalia kwa jicho la huruma akinamama wanaouza vyakula katika eneo la hospitali hiyo, akipendekeza wapewe maeneo rasmi yenye kivuli ili kufanya shughuli zao katika mazingira bora na salama.
Mavunde pia ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau waliomsaidia kufanikisha ujenzi huo, akiwemo Mkurugenzi wa Asasi ya Salim Asasi, mchezaji wa Yanga Stephane Aziz Ki, kipa wa Yanga Djigui Diarra na mfanyabiashara Vencampan ambao waliwezesha takriban asilimia 80 ya gharama za ujenzi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,  Rosemery Senyamule, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alieleza kuwa jengo hilo ni ukombozi na faraja kwa familia nyingi zinazouguza wapendwa wao hospitalini, huku akimpongeza Mbunge huyo kwa moyo wake wa huruma na utekelezaji wa ahadi kwa vitendo.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Ibenzi Ernest, amesema mchango wa Mbunge Mavunde ni wa kipekee na umeleta matumaini makubwa kwa hospitali hiyo ambayo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa watumishi na uzio wa kuzunguka eneo lote.
“Dira yetu ni kutoa huduma bora kwa wananchi. Mchango kama huu si tu unatuongezea uwezo bali pia unatuonyesha kuwa jamii inatambua na kushiriki katika jitihada za maboresho,” a.esema Dkt. Ernest.
Kwa matendo haya, Mbunge Mavunde ameendelea kuonesha kuwa uongozi wa kisasa unahitaji maono, moyo wa kujitoa na uwezo wa kutekeleza ahadi kwa vitendo  mfano bora kwa wanasiasa wanaotaka kujenga historia ya kweli kwa jamii.

About the author

mzalendoeditor