Featured Kitaifa

MABILIONI YA CSR KUTOKA BARRICK BULYANHULU KUTEKELEZA MIRADI YA ELIMU, AFYA NA UWEKEZAJI HALMASHAURI YA MSALALA 2025

Written by mzalendoeditor
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Msalala, Mibako Mabubu (Kushoto) akibadilishana mkataba wa makubaliano na Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Charles Mhando ,wengine pichani ni wafanyakazi wa halmashauri hiyo na Mgodi wa Bulyanhulu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Msalala Leonard Mashaka Mabula (Kushoto) akibadilishana mkataba wa makubaliano na Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Charles Mhando
Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu,Charles Mhando akiongea katika hafla hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Msalala ,Mibako Mabubu akiongea katika hafla hiyo
Picha ya pamoja baada ya zoezi la kusaini mkataba wa makubaliano
**
Uwekezaji wa kampuni ya Barrick nchini yenye ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals, unazidi kuleta manufaa kwa wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala iliyopo mkoani Shinyanga ambapo mwaka huu Mgodi wake wa Barrick Bulyanhulu utatoa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) kiasi cha shilingi bilioni mbili na milioni mia moja na hamsini kwa ajili ya utekelezaji miradi ya afya,elimu na uwekezaji.
Hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano imefanyika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala na kuhudhuriwa na viongozi,wataalamu mbalimbali na baadhi ya Wafanyakazi kutoka mgodi wa Barrick Bulyanhulu.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Mibako Mabubu amebainisha kuwa baadhi ya miradi itakayotekelezwa katika kipindi cha mwaka huu wa 2025 ni ujenzi wa uzio kwenye mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Segese A, Ujenzi wa nyumba ya Mwalimu mlezi shule ya msingi Segese A, Ununuzi wa vifaa na vitendea kazi kwa ajili ya ofisi na madarasa katika chuo cha afya Ntobo na ukamilishaji wa bweni Shule ya Sekondari Kashishi .
Mingine ni ujenzi wa shule ya Shikizi Kijiji cha Ilogi vyumba 4 vya madarasa na matundu 8 ya vyoo vya wanafunzi na matundu 2 ya vyoo vya Walimu pia kukamilisha Jengo la Abiria katika kituo cha mabasi cha Segese.
Mabubu ametoa wito kwa Wataalamu wa halmashauri hiyo kusimamia vizuri maradi hiyo ili iwe na viwango vinavyotakiwa na itekelezwe na kumalizika kwa wakati ili wananchi walengwa waweze kuanza kunufaika nao.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Msalala Leonard Mashaka Mabula, amesema ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya CSR katika wilaya hiyo umekuwa ukizidi kuwa bora mwaka hadi mwaka na kwa sehemu kubwa utajikita kwenye miradi ya kijamii ambayo ni vipaumbele vya wananchi wa maeneo husika.
“Mpango wa utekelezaji wa Miradi hii ni shirikishi na inafanywa baada ya kupata mawazo ya wananchi na madiwani ambao ndio wawakilishi wao, na maelekezo ni kwamba mipango yote ijikite katika kutatua kero za wananchi na vipaumbele vyao”,amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Charles Mhando,amesema Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, utaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha fedha za CSR zinazotolewa na Mgodi huo kila mwaka zinaendelea kuwaletea maendeleo wananchi na kufanya maisha yao kuwa bora ili wanufaike na uwekezaji wa mgodi na uwepo mgodi kwenye wilaya yao.

About the author

mzalendoeditor