Katika kuimarishaji hifadhi ya haki za binadamu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imefanya zoezi la upandaji miti katika eneo la wazi lililopo mtaa wa Salama kata ya Nkuhungu mkoani Dodoma.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mohamed Hamis Hamad amesema mojawapo ya haki ya binadamu ni kuishi katika mazingira safi na salama.
“Sisi tume tumeamua kuimarisha haki hii kwa vitendo kwa kupanda miti katika eneo hili tangu mwaka mwaka 2022 na leo tumekuja kuendeleza sehemu nyingine iliyokuwa imesalia ili kuimarisha hifadhi ya haki za binadamu na utawala bora kwa vitendo kabisa “amesema.
Aidha, ameipongeza Serikali kwa kuhimiza uhifadhi wa mazingira, na kuongeza kuwa THBUB kama mdau mkubwa wa haki za binadamu wanafahamu changamoto mbalimbali zilizopo nchini kuhusu uhifadhi wa mazingira hivyo wao kwa kufanya hivyo wanatambua kuwa hiyo ni haki muhimu.
Pia amewatoa hofu wananchi kuhusiana na uleaji wa miti hiyo kutokana na sasa Dodoma kuwa katika kipindi cha kiangazi, hivyo amesema watahakikisha wanamwagilia maji kila siku ili kuhakikisha miti hiyo inastawi na kuleta tija kwa wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Salama kata ya Nkuhungu Habas Mwijuki ametoa wito kwa wananchi wa mtaa huo kupanda miti katika maeneo yao pamoja na kuitunza ili iwe endelevu na kubadilisha mazingira ya Dodoma iweze kuwa ya kijani.
“Hii miti imesaidia katika mazingira yetu kwanza imepunguza upepo uliokuwa unavuma kwa kasi sana katika eneo hili hasa wakati wa kiangazi, lakini wananchi wangu wanapata sehemu safi ya kuweza kupumzika na mazingira yameboreshwa na kuwa safi,”amesema.
Naye Balozi wa Mazingira Mkoa wa Dodoma Julian Bruno ameipongeza THBUB kwa kufanya zoezi hilo katika kuhakikisha ustawi wa binadamu kuhakikisha uhai wa binadamu unaendelea kuwepo.