Featured Kitaifa

DKT.TAUSI KIDA AKAGUA JENGO LA OFISI MPYA MTUMBA, ATOA WITO WA KUKAMILIKA KWA WAKATI

Written by mzalendoeditor

Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, leo amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi hiyo lililopo Mtaa wa Ardhi, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Katika ukaguzi huo, Dkt. Kida amemwelekeza mkandarasi anayejenga mradi huo, Suma JKT, kukamilisha ujenzi na kukabidhi jengo hilo mapema iwezekanavyo kwa kuwa serikali imekamilisha sehemu kubwa ya malipo anayostahili mkandarasi huyo,

Aidha, alikumbusha mhandisi mshauri, ambaye ni Chuo Kikuu cha Ardhi, kuhakikisha anasimamia ubora ili jengo hilo liwe na hadhi na viwango vya juu vinavyoendana na thamani halisi ya fedha za Serikali.

Kwa sasa, mradi wa ujenzi wa jengo hilo upo katika hatua za mwisho ambapo imeelezwa kuwa umefikia asilimia 77. Jengo linatarajiwa kukabidhiwa rasmi Septemba, mwaka huu.

About the author

mzalendoeditor