Featured Kitaifa

KUNAMBI: ASANTE RAIS SAMIA KWA MRADI MKUBWA WA MAJI NA BARABARA YA LAMI MLIMBA

Written by mzalendoeditor

MBUNGE wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro, Godwin Kunambi amejumuika pamoja na Viongozi wa Dini, Chama Cha Mapinduzi na Wananchi wa Tarafa ya Mlimba katika Dua Maalum ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan iliyofanyika katika Msikiti wa Masjid Taqwa katika Tarafa hiyo.

Akizungumza baada ya Dua na Futari hiyo maalum, Kunambi amesema Rais Samia amefanya mambo makubwa katika Jimbo la Mlimba kwenye miezi 14 yake ya uongozi ikiwa ni pamoja na kutoa kibali cha kuanza kwa ujenzi wa Barabara ya Lami yenye Kilomita 50 itakayounganisha Halmashauri ya Manispaa ya Ifakara na Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba.

Amesema mbali na Rais Samia kutoa kibali cha ujenzi wa Barabara hiyo pia amewapatia kiasi cha Sh Bilioni 3.7 za mradi wa maji mserereko ambao utakwenda kumaliza changamoto ya Maji katika Tarafa hiyo.

” Tuna Kila sababu ya Kumuombea Rais Samia kwa mambo makubwa aliyoyafanya kwenye Jimbo letu, mpaka Sasa ameshaidhisha kuanza kwa ujenzi wa Barabara ya Lami ya Kilomita 50 ambayo itaunganisha Mlimba na Ifakara jambo ambalo litatusaidia kufungua zaidi fursa za kibiashara.

Kupitia Rais Samia pia tumefanikiwa kupata Barabara ya kiwango cha Lami kutoka Kihansi Mlimba hadi Madeke ambapo ni mpakani mwetu na Mkoa wa Njombe, Barabara hii inafanyiwa usanifu na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Tunaamini kupitia Barabara hii biashara kati yetu na Njombe itakua kubwa zaidi ambapo sisi tutatoa Mbao kwao kwa bei rahisi na wao watanunua zaidi Mchele kutoka kwetu,” Amesema Kunambi.

Amesema pia Rais Samia amesikia kilio cha wananchi wa Mlimba cha kero ya Maji na tayari ameshaidhisha kiasi cha Sh Bilioni 3.7 kwa ajili ya utatuzi wa changamoto hiyo.

” Rais wetu ni msikivu sana anajua changamoto ya Maji inayotukabili, tunavyozungumza sasa tayari ametupatia Sh Bilioni 3.7 kwa ajili ya mradi mkubwa wa Maji utakaohudumia wananchi wote wa Tarafa hii ya Mlimba na shughuli za uungaji mabomba zimekamilika, hivyo suala la kero ya maji Mlimba Sasa linakwenda kuwa Historia,” Amesema Kunambi.

About the author

mzalendoeditor